Rais Donald
Trump amemkosoa Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer kwa mara ya pili wiki
hii, akisema "inasikitisha kuona" uhusiano wa kipekee ukiharibika
baada ya Uingereza kusita kutoa msaada kwa mashambulizi ya Marekani dhidi ya
Iran.
Starmer amesema
Uingereza haikushiriki katika shambulizi dhidi ya Iran lililofanywa na Marekani
na Israeli kwa sababu hatua yoyote ya kijeshi ya Uingereza lazima iwe na
"mpango unaofaa uliotathminiwa vyema" na hakuamini katika "kupinduliwa
kwa serikali kupitia nguvu ya nje".
Lakini tangu
wakati huo ameruhusu Marekani kutumia kambi za Uingereza kuanzisha kile
alichokiita mashambulizi kidogo ya kujilinda ili kudhoofisha uwezo wa
Iran, ambayo imewashambulia washirika wa Marekani katika eneo hilo kwa ndege
zisizo na rubani na makombora.
Siku ya
Jumatatu, kambi ya Uingereza huko Cyprus ilishambuliwa na ndege isiyo
na rubani ambayo maafisa wa Cyprus walisema huenda ilirushwa na kundi la
Hezbollah la Lebanon linaloungwa mkono na Iran.
Trump
alisema hakuhitaji msaada wa Uingereza kuishambulia Iran lakini akaongeza kuwa
kusuasua huko kumeikatisha tamaa.
"Inasikitisha
sana kuona kwamba uhusiano huu si kama ulivyokuwa," Trump aliambia gazeti
la Sun katika mahojiano yaliyochapishwa Jumanne.
Aliambia
Telegraph siku ya Jumatatu kwamba Starmer alionekana kuwa na "wasiwasi
kuhusu uhalali" wa mashambulizi dhidi ya Iran, alipoanza kufikiria iwapo ataruhusu
kambi muhimu ya kijeshi ya Uingereza, Diego Garcia, itumike.
Akizungumza
na gazeti la Sun, Trump alisema kwamba hajawahi kufikiria kuwa angeiona
Uingereza ikiwa mshirika wa kusuasua, na badala yake alizisifu Ufaransa na
Ujerumani.
"Huu
ulikuwa uhusiano imara zaidi kuliko wote," alisema. "Na sasa tuna
uhusiano imara sana na nchi zingine barani Ulaya."
"Ufaransa
imekuwa bora. Wote wamekuwa wazuri. Uingereza imekuwa tofauti sana na nchi zingine."
Uingereza,
Ufaransa na Ujerumani zote zilitoa taarifa ya pamoja kujibu mashambulizi
ya Iran siku ya Jumamosi, zikisema kwamba zilikuwa na mawasiliano ya
karibu na Marekani, Israel na washirika wake katika eneo hilo, na zikatoa wito
wa kuanza tena kwa mazungumzo.
Starmer
amekosolewa kutoka pande zote za nyumbani kwa uamuzi huo, huku wapinzani upande
wa kushoto wakimtaka alaani kitendo hicho cha kijeshi na upande wa kulia,
viongozi wa upinzani Kemi Badenoch na Nigel Farage wakimshambulia Starmer kwa
kushindwa kumuunga mkono mshirika mkuu wa usalama na ujasusi wa Uingereza.