Kifo cha Costa Titch: Rapper wa Afrika Kusini 'alitaka kufikia kiwango cha juu zaidi'

Tich

Chanzo cha picha, Getty Images

Costa Titch alikuwa na mipango mikubwa na ndoto kubwa.

Lakini, Jumamosi, mashabiki wa rapa huyo wa Afrika Kusini walihofia hali mbaya zaidi alipoanguka jukwaani.

Baadaye, familia yake ilithibitisha: "Kifo kilibisha mlango wetu kwa bahati mbaya," katika taarifa kwenye Instagram.

Salamu za rambi rambi zimetolewa kwa kijana huyo mwenye umri wa miaka 28 huku polisi wakichunguza kilichotokea.

Mtangazaji wa BBC 1Xtra Jeremiah Asiamah, ambaye alimhoji Costa Titch wiki chache zilizopita, anasema ni " pigo kubwa sana".

"Sio tu kwa sauti ya amapiano, lakini kwa wale wote wanaofurahia muziki mzuri," anaiambia BBC Newsbeat.

"Anapopanda jukwaani, uwepo wake unavutia - kama muziki wake."

Costa Titch alikuwa nani?

Jina lake halisi ni Constantinos Tsobanoglou, lakini alijulikana kama Costa Titch katika ulimwengu wa burudani. Alianza kazi yake kama dansi, kabla ya mafanikio makubwa ya kimataifa mnamo 2022 na wimbo wake Big Flexa.

Mwezi uliopita, alitangaza ushirikiano na lebo ya rekodi ya Akon Konvict Kulture.

Rapa hao walishirikiana kwenye remix ya wimbo huo - uliopewa jina la 'Rising Record' kwenye Rave Show ya 1Xtra.

"Kama vile ile ya awali ilifanya vyema, bado kuna sehemu nyingi duniani ambazo hazijasikia kuhusu rekodi hiyo," Costa aliambia kipindi hicho.

Titch

Chanzo cha picha, Jeremiah Asiamah

Lakini kulingana na Jeremiah, matarajio ya Costa yalikwenda zaidi ya wimbo mmoja.

"Tulipokuwa tunazungumza, aliniambia, 'Big Flexa imefanya vyema, lakini nataka kuipeleka kwenye ngazi mpya kabisa - nataka kuwaonyesha watu kuwa mimi ni zaidi ya rapa, mimi ni zaidi ya mchezaji tu, mimi ni mwanamuziki."

Amapiano ni nini?

Jeremiah anaeleza kuwa amapiano ni tanzu ya muziki wa klabu ambao iliibuka kutoka Afrika Kusini.

Anasema "imechangiwa na burudani za klabuni, jazba, muziki wa mapumziko, na kuwianisha sauti hizo zote pamoja kwa ngoma za furaha na za kipekee."

"Kama ungepata nafasi ya kumuona Costa Titch moja kwa moja, kila mtu alikuwa akifanya ngoma zake."

Na akitoka kwenye malezi ya kucheza dansi, "unaweza kufikiria tu athari aliyokuwa nayo kwenye amapiano," Yeremia anaongeza.

Alikufa vipi?

Video kwenye mitandao ya kijamii zinamuonyesha Costa akiwa ameanguka mara mbili kabla ya kushuka jukwaani, alipokuwa akitumbuiza kwenye tamasha la Ultra Afrika Kusini mjini Johannesburg.

Waandaaji walimtaja kama msanii "mpendwa" na "sauti ya kuvutia miongoni mwa wasanii wa amapiano la Afrika Kusini".

Walisema "wamehuzunishwa na kifo chake cha ghafla".

Licha ya uvumi mtandaoni, hakuna sababu za kifo zilizotolewa.

Polisi wa eneo hilo wanasema hili litathibitishwa na uchunguzi wa maiti, na familia ya Costa imeomba "wakati na nafasi" huku "wanajaribu kupata maana ya kile ambacho kimetupata".

'Muziki wao utaendelea kuvuma'

Costa alifariki mwezi mmoja tu baada ya rapa mwenzake wa Afrika Kusini AKA, ambaye polisi wanasema aliuawa.

"AKA na Costa Titch walikuwa marafiki wa karibu sana," anasema Jeremiah.

 Kifo cha Costa Titch (kulia) kimekuja mwezi mmoja baada ya kuuawa kwa rafiki yake na rapa mwenzake kutoka Afrika Kusini AKA (kushoto)

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Kifo cha Costa Titch (kulia) kimekuja mwezi mmoja baada ya kuuawa kwa rafiki yake na rapa mwenzake kutoka Afrika Kusini AKA (kushoto)

"Inasikitisha sana kwamba Afrika Kusini na watu kote duniani ambao walipenda muziki wa wasanii hawa wawili wamewapoteza.

"Lakini - najua faraja ya ni kwamba - muziki wao utaendelea," Jeremiah anasema.

"Nyimbo zao sasa zitavuma zaidi katika vilabu - watu watasherehekea maisha yao, kwa sababu najua hicho ndicho wangependa kutoka kwetu."