Je, huu ni msimu wa Arsenal wa kumaliza ukame wa Ligi kuu ya Epl?

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Wachezaji wa Arsenal Eze na Hincapie
    • Author, Ahmed Omar Bahaj
    • Nafasi, BBC Swahili
    • Akiripoti kutoka, Nairobi Kenya
  • Muda wa kusoma: Dakika 3

Kinyang'anyiro cha ligi ya soka ya Premier chazidi kupamba moto

Je, Arsenal ataumaliza mwendo ashinde taji la ligi ya Epl?

Je, huu ni msimu wa Arsenal wa kumaliza ukame wa Ligi kuu ya Epl?

Matumaini ya Arsenal ya kumaliza ukame wa miaka 21 wa kushinda kombe la ligi kuu ya Epl nchini England yamefufuka upya baada ya kuvuna ushindi katika mechi zake mbili zilizopita tena zote za debi la London.

Kwanza Walimtitiga Tottenham 4-1 alafu wakamkaranga Chelsea 2-1 ,zote hizi zikiwa mechi ngumu.

The gunners bado wako kileleni mwa jedwali la EPL wakiwa na alama 64, kwa jumla wanaongoza kwa alama 5, lakini hii baada ya kucheza mechi 29 ikiwa ni mechi moja zaidi ya washindani wao Manchester City walio nyuma yao kwa karibu katika nafasi ya pili wakiwa na alama 59.

Pep Guardiola wa City anasubiri kwa hamu Arsenal ateleze tena tu apoteze alama ,ili ambakure nyama mdomoni, lakini Mikel Arteta na vijana wake ndio mwanzo wamepata ari mpya ya kupambania taji kufa kupona.

Ubashiri wa SUPERCOMPUTER YA Opta unasemaje?

Tovuti mashuhuri ya kimataifa ya uchambuzi YA SUPERCOMPUTER YA OPTA ,inabashiri kuwa nafasi za Arsenal kushinda ligi msimu huu zimepanda kutoka asilimia 82 hadi 88.

Nao Man City fursa zao za kushinda ligi zipo kwa asilimia 16.62.

Aston villa wamepewa asilimia 0.08 kushinda , Manchester United pia wapo japo kwa asilimia kiduchu ya 0.02.

Hebu tuchambuwe kwa uhalisia wa mechi zijazo

Mechi tano sijazo za Arsenal

Hizi hapa mechi tano zijazo za Arsenal

kwanza Brighton Albion ugenini

Kisha Everton nyumbani Emirates

Alafu Bournemouth nyumbani Emirate

Sasa mechi kubwa itakayoamua mbivu na mbichi kuhusu taji msimu huu ni hili dimba la Arsenal dhidi ya Manchester city tarehe 18 Aprili tena city akiwa nyumbani Etihad.

Iwapo Arsenal atafanikiwa kumbamiza City kwenye mechi hii basi ataukata mzizi wa fitina baina yao na kwa hakika atakuwa amenusa harufu ya taji, kwani zitasalia mechi 5 tu kutoka hapo kabla ligi iishe.

.

Chanzo cha picha, Getty

Maelezo ya picha, Mkufunzi wa Man City Pep Guardiola

Mechi tano zijazo za CIty

Upande wa Manchester City,mechi zao tano zijazo ni dhidi ya Nottingham forest,West ham,Crystal Palace,Chelsea na Arsenal.

Hata hivyo kumeibuka mjadala siku za hivi karibuni kuwa arsenal wanashinda mechi zao kwa njia zisizovutia ,mfano wameshinda mechi 10 kupitia mipira ya kona na mipira mifu.

Sasa baadhi wa makocha kama Ann slot wa Liverpool,David Moyes wa Everon na hata Michael Carick wa Man United wameanza kulalamika kuwa eti arsenal wanatumia mabavu kushinda.Sidhani kama malalamiko haya yana mashiko yoyote.

'Nimewaambia vijana wangu wasipoteze muelekeo' - Arteta

.

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Mkufunzi wa Arsenal MIkel Arteta

Kwani upande wake Mikel Arteta anasemaje ?

'Nimewaambia vijana wangu wasipoteze muelekeo,kila mmoja atasema lake, cha muhimu ni kushinda mechi zetu.'Alisema Arteta

Arsenal mara mwisho kushinda ligi kuu ya Premier ni mwaka 2004 ,walishindwa bila kupoteza hata mechi moja chini ya mkufunzi Arsene Wenger.

Arsenal sasa wamebakisha mechi 9 tu kumaliza ligi ya EPL na kwao kila mechi sasa ni kama fainali wakitumai mambo ni kangaja na huenda yakaja safari hii.

SYote tisa la kumi ni ,je hatimaye huu ndio msimu wa Arsenal wa kuikata kiu ya miaka 21 ya kushinda taji la ligi kuu ya epl?

Ama man city watakitia kitumbua chao mchanga na kuiharabia sherehe?

Kila mbuzi mbuzi atakula kwa urefu wa Kamba yake.