Kwanini Iran haijamshambulia jirani yake Uturuki licha ya kumiliki kambi za kijeshi za Marekani?

Chanzo cha picha, EPA
Uharibifu na vifo vinavyotokana na vita vilivyoanza tarehe 28 mwezi Februari baada ya Marekani na Israel kuishambulia Iran inazidi kuongezeka.
Iran kwa kujibu shambulio hilo imelenga miundombinu tofauti nchini Kuwait,Saudi Arabia,Oman,Bahrain,Qatar,Jordan,Iraq,Cyprus na Falme za Kiarabu.
Taifa la Uturuki ambalo liko karibu na rasi ya kiarabu ni miongoni mwa mataifa chache ambayo hayajalengwa na Iran.
Wataalam waliozungumza na BBC wanasema licha ya Uturuki kuwa na kambi za kijeshi za Marekani na kuwa mwanachama wa Jumuiya ya kujihami ya Nato, bado haijalengwa.
Wataalam hao wanahoji kuwa Ankara na Tehran wana uhusiano mzuri na labda imechangia wao kutolengwa na mashambulizi ya kulipiza kisasi ya Iran.
Uturuki imekashifu mashambulizi ya Marekani na Israel dhidi ya Iran, na pia kuishtumu Iran kwa kujibu mashambulizi hayo.
Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan, alisema tarehe 28 mwezi Februari kuwa taifa hilo litaimarisha diplomasia yake ili kuepuka vita.
Uanachama wa Nato
Sinan Ulgen, rais wa kituo cha utafiti wa Sera za uchumi na za kigeni (EDAM), anasema kuwa uanachama wa Uturuki katika NATO ndio jambo linaloitofautisha nchi hiyo na mataifa mengine yanayolengwa na Iran katika eneo hilo.
Akizungumza na BBC Turkish, alisema kwamba shambulio lolote la aina hiyo ndani ya mfumo wa kifungu cha 5 cha Mkataba wa NATO, inaamanisha kuwa kuilenga Uturuki kunachukuliwa kama kulenga nchi zote ambao ni wanachama wa muungano huo.
Ulgen anaamini kuwa Iran itaepuka kutanua mzozo unaoendelea kwa kutolenga kambi za kijeshi za Marekani nchini Uturuki. Aliongezea kuwa "Iran haitataka kuongeza eneo lingine la vita karibu na eneo lake, kwa kuishambulia Uturuki, wala haitataka kuchokoza nchi yenye nguvu kubwa ya kijeshi na uwezo wa juu wa kujizuia. Kwa hiyo, nadhani uwezekano wa shambulio la moja kwa moja la Iran dhidi ya Uturuki ni mdogo sana."
Aidha Kambi ya anga ya Incirlik iliyoko Adana haikutumika katika mashambulizi dhidi ya Iran.

Chanzo cha picha, Eren Bozkurt/Anadolu Ajansı/Getty Images
Kwa upande wake, mtafiti Oral Tuga kutoka Kituo cha utafiti cha Iran (İRAM) anaamini kuwa uwezekano maeneo tofauti ya Uturuki kulengwa katika mashambulizi ya kulipiza kisasi ya Iran ni mdogo.
Akizungumza na BBC News Turk, alisema:
"Labda kundi fulani ndani ya Iran litachukua hatua yao binafsi kuanzisha mashambulizi, jambo ambalo naliona kuwa haliwezekani.Sidhani kama Tehran itachukua mkondo huo wa kuanzisha vita dhidi ya nchi mwanachama wa NATO na kufanya hali kuwa ngumu zaidi kwao."
Tuga anaeleza kuwa Uturuki na Iran, ambao wanampaka mmoja wenye urefu zaidi ya kilomita 500, na wanashirikiana kwa kutegemeana
"Raia wa Iran, hasa baada ya kifo cha aliyekuwa Rais wa zamani wa Iran Ebrahim Raisi, wamekuwa wakijitahidi kuimarisha ushirikiano wao wa kimkakati na Uturuki, na sioni wakibadili mwelekeo wao"
Kambi za Incirlik and Kurcik
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Uturuki imedhibitisha kuwa anga zake hazikutumiwa, na kambi ya kijeshi ya Marekani iliyoko nchini humo pia haikutumiwa kutekeleza mashambulizi dhidi ya Iran.
Katika taarifa iliyotolewa tarehe 28 Februari na kituo cha kupambana na taarifa potofu, kinachohusishwa na mkurugenzi ya mawasiliano ya ofisi ya rais wa Uturuki, ilisema kuwa Ankara hairuhusu anga yake au rasilimali zinazohusiana nalo kutumika "kwa madhumuni ya kijeshi" katika "mzozo au vita vyovyote ambavyo hawahusiki navyo."
Kambi ya Anga ya Incirlik na kambi ya Kürecik iliyoko Malatya ni miongoni mwa vituo muhimu zaidi vya kijeshi vinavyohusishwa na Marekani nchini Uturuki.
Kulingana na tovuti rasmi ya kambi ya anga ya Incirlik, kituo hicho kilianzishwa mwaka 1951 na timu iliyojulikana kama "American Engineering Group."
Mwaka 1954, makao makuu ya jeshi la Uturuki na Jeshi la anga la Marekani walitia saini makubaliano ya matumizi ya pamoja ya kambi hiyo, na uendeshaji wake unasimamiwa chini ya "mkataba wa ushirikiano wa ulinzi " uliosainiwa kati ya Marekani na Uturuki mwaka wa 1980.
Wizara ya Ulinzi ya Uturuki inasema kuwa kambi hiyo iko chini ya mamlaka ya jeshi la Uturuki, na kwamba inamilikiwa na Jamhuri ya Uturuki.
Kuhusu kambi ya Kürecik, iliyoko katika wilaya ya Akçadağ, mashariki mwa mkoa wa Malatya, ni kituo cha tahadhari ya mapema kilichoanzishwa mwaka 2012 na kinafanya kazi chini ya mfumo wa NATO.
Mwaka 2011, aliyekuwa Rais wa Iran wakati huo, Mahmoud Ahmadinejad, alikosoa kuanzishwa kwa kambi hiyo, akidai kuwa iliwekwa kwa lengo la kuilinda Israel dhidi ya mashambulizi ya makombora ya Iran yanayoweza kutokea.

Chanzo cha picha, Getty Images
Suala la kutafuta hifadhi
Miongoni mwa athari zinazoweza kujitokeza wakati wa vita kati ya Marekani na Israel kwa upande mmoja na Iran kwa upande mwingine, ni idadi kubwa ya wakimbizi ambao watakimbilia Uturuki kutoka Iran.
Ankara na Tehran zilitangaza tarehe 2 mwezi Machi kusitisha kwa pamoja usafiri wa abiria katika mpaka wao. Waziri wa biashara wa Uturuki, Ömer Polat, alisema kuwa nchi hizo mbili zitaruhusu raia wao kurejea makwao, huku Uturuki ikiendelea kuweka mipaka yake wazi kwa raia wa nchi zingine walioko kwa sasa nchini Iran.
Sinan Ülgen, anaamini kuwa hali mbaya zaidi kutokea kwa Uturuki ni kukosekana kwa amani nchini Iran, jambo ambalo linaweza kusababisha kama ilivyotokea Iraq na Syria, watu wengi kukimbilia mpaka wa Uturuki.















