Fahamu vifaa 6 vya kipekee vilivyobuniwa na wanawake duniani

Chanzo cha picha, Getty Images
Ukulizwa kuhusu wavumbuzi maarufu duniani, majina kama Thomas Edison, aliyevumbua balbu ya taa, na Alexander Graham Bell, aliyevumbua simu, huja akilini mara moja.
Lakini si wavumbuzi wanawake.
Je, unawafahamu wavumbuzi wanawake kama Mary Anderson au Ann Tsukamoto?
Huenda usiyajue majina haya, lakini wanawake hawa walibudi na kuunda vifaa vilivyotoa mchango mkubwa katika sayansi dunaini na ambavyo tunavitumia kila siku.
1. Grace Hopper- Muundaji wa Programu ya Kompyuta

Chanzo cha picha, Getty Images
Baada ya kujiunga na Jeshi la Wanamaji la Marekani wakati wa Vita kuu ya pili ya dunia, Grace Hopper alipewa jukumu la kuja na ubunifu wa kompyuta mpya iitwayo Mark1. Alianzisha umahiri wake katika programu za kompyuta katika miaka ya 1950.
Aliunda lugha ya kompyuta iliyotafsiri maagizo inayopewa na mtumiaji kuwa lugha ambayo kompyuta inaweza kuelewa na kusoma. Hii hatimaye ikawa maendeleo makubwa kwa jinsi kompyuta zilivyofanya kazi. Hopper pia alichangia katika neno maarufu la "de-bugging," ambalo linamaanisha kurekebisha makosa na bado linatumika sana ulimwenguni kote hadi leo.
Grace alifanya kazi za kompyuta hadi alipostaafu, na kuwa afisa mzee zaidi aliyewahi kutumikia katika Jeshi la Wanamaji la Marekani. Alikuwa na umri wa miaka 79 alipostaafu.
2. Namba ya kupiga na kusubiri - Dk. Shirley Ann Jackson

Dk. Shirley Ann Jackson ni mwanafizikia wa Marekani. Utafiti wake tangu miaka ya 1970 umesababisha mapinduzi katika mawasiliano. Ugunduzi wa kutambua anayekupigia hata kama hayuko kwenye kumbukumbu za simu yako (caller ID) kumsubirisha kwenye simu mtu na pengine.
Ubunifu wake wa mawasiliano pia uliwawezesha wengine kutengeneza mashine za faksi zinazobebeka, nyaya za fiber optic, na sahani zinazotumia nishati ya jua. Alikuwa mwanamke wa pili mweusi kupata shahada ya uzamivu (PhD) na wa kwanza kutoka Taasisi ya Teknolojia ya Massachusetts na pia akawa mwanamke wa kwanza wa Marekani kuongoza timu ya utafiti ya juu ya chuo kikuu hicho.
3. Mary Anderson - Vifuta vioo vya gari (Car Windshield Wipers)

Chanzo cha picha, Getty Images
Mnamo 1903, Mary Anderson, alipotembelea Jiji la New York, aligundua kuwa dereva ilimbidi afungue madirisha ili kuondoa barafu kwenye kioo cha mbele. Kila mara dirisha lilipofunguliwa, abiria wa gari walihisi baridi.
Kwa hivyo Anderson alikuja na suluhisho: kifaa cha mpira chenye ncha kali ambacho kingeondoa barafu kwenye kioo.
Mnamo 1903, alipewa hati miliki kwa uvumbuzi wa kifaa hiki. Anderson hakuwahi kufaidika na uvumbuzi wake, hata baada ya vifaa hivi kutapakaa kila mahali sasa na kila gari inavyo na vimekuwa vya kawaida kwenye kila gari.
4. Olga D Gonzalez-Sanabria - Betri za Satelaiti
Betri zenye maisha marefu ama zinazokaa kwa muda mrefu zaidi zinazotumika kuwasha satelaiti kwenye anga za mbali zimeanzia kwa Olga. Ni vifaa muhimu sana.
Olga D Gonzalez-Sanabria anatoka Puerto Rico, na aligundua teknolojia iliyotumika kutengeneza betri hizi mnamo 1980.
Baadaye alikuja kuwa mkurugenzi wa Kituo cha Utafiti cha Glenn cha NASA.
5. Josephine Cochrane - Mashine ya kuoshea vyombo (Dishwasher)

Chanzo cha picha, Getty Images
Cochrane alitaka mashine ambayo ingeosha vyombo haraka kuliko mfanyakazi ambaye ni binadamu na ambayo haingeweza kuharibika kwa urahisi.
Mashine aliyoiunda ilikuwa mashine inayoendeshwa kwa miguu iliyounganishwa na mota inayozunguka, na ikawa mashine ya kwanza kutumia maji kama nguvu ya kuisaida kufanya kazi. Mume wa Cochrane alikuwa mlevi mkubwa na alifariki akimuachia madeni mengi ya kulipa, jambo lililomfanya atumie uvumbuzi wake mnamo 1886 kwa kuanzisha kiwanda cha kutengeneza kifaa hicho ama mashine hiyo ambayo baadaye iliboreshwa na wengine na kuwa kifaa muhimu kwa maisha ya binadamu.
6. Marie Van Brittan Brown – Vifaa vya usalama wa nyumbani

Chanzo cha picha, Getty Images
Marie Van Brittan Brown, muuguzi ambaye mara nyingi alikuwa anakaa nyumbani peke yake, mumewe akienda kwenye shughuli za kujitafitia kipato, alikuja na wazo la kuuunda kitu ili awe salama akiwa nyumbani kwake peke yake. Yeye na mumewe Albert wakaanza kuuunda mfumo wa kwanza wa usalama wa nyumbani. Sababu ya kuunda kifaa hiki ilitokana na miaka ya 1960, ambapo uhalifu ulikuwa ukiongezeka na polisi walikuwa wakichelewa kushughulikia.
Kifaa walichokiunda kilikuwa kifaa cha kisasa chenye kamera zilizounganishwa kwenye mlango wa nyumba. Walifuatilia kutoka kwenye skrini chumbani kwake, ambayo ilikuwa na kengele ya mlango. Uvumbuzi huu ukawa msingi wa CCTV Camera ambazo leo zimetapakaa duniani kote.













