Francis Ngannou: Mhamiaji haramu kutoka Afrika atakaye zichapa na Tyson Fury kesho

Chanzo cha picha, Getty Images
- Author, Papa Atou Diaw
- Nafasi, BBC
Tarehe 28 Oktoba 2023, Francis Ngannou almaarufu "The Predator" atamenyana na bingwa wa ndondi wa uzito wa juu, Mwingireza, Tyson Fury huko Riyadh, Saudi Arabia.
Mechi ya ndondi ambayo hakuna mtu aliifikiria miaka michache iliyopita.
Je, Francis Ngannou ataweza kumshinda Tyson Fury ambaye hajawahi shindwa? Hili ndilo swali ambalo mashabiki wengi wa michezo huu wanajiuliza.
Francis Ngannou atapigana na Mfalme wa Gypsy. Mkameruni huyo ameibuka kutoka katika mchezo unaojumuisha aina zote za mapigano, ndondi, mateke, mieleka, ngumi. Wakati Tyson Fury ni mwanandondi - anayetumia ngumi pekee.
"Kitaalamu itakuwa ngumu kwa Francis Ngannou ambaye amezoea MMA - kukabiliana na bondia bora zaidi duniani," anaeleza Léandre Nzie, mwandishi wa habari wa Cameroon.
Kukulia Cameroon

Chanzo cha picha, Getty Images
Francis Ngannou alizaliwa katika familia masikini. Akiwa mdogo vizuizi vya maisha vilimsukuma kuchukua majukumu mapema sana ambayo watoto wa rika lake wasingeweza kuyabeba - akifanya kazi katika mgodi wa mchanga.
“Nilikuwa na umri wa miaka 10 nilipoanza kwa sababu nilikuwa kijijini nilikokulia. Baada ya kuondoka nyumbani kwetu, nilienda kwa bibi yangu. Iinibidi kufanya kazi ili kuchangia huduma za nyumbani; kununua mafuta, chakula na kwa masomo kununua vitabu,” anaeleza Francis Ngannou katika kipindi cha mtandaoni cha Joe Rogan.
"Lazima ufanye kazi na hivyo ndivyo nilivyoanza, ingawa kazi hii ilikuwa ya watu wazima, lakini sikukuwa na chaguo jingine," anaelezea bingwa huyo wa zamani wa Ultimate Fighting Championship (UFC).
Francis Ngannou alifanya kazi katika migodi ya mchanga hadi alipokuwa na umri wa miaka 17.
Kadiri umri ulivyosonga, matatizo yaliendelea kurundikana kwenye mabega ya Francis ambaye anataka jambo moja tu: kutimiza ndoto ya kuwa bingwa wa ndondi.
Kwahiyo aliamua kuhamia Ulaya kwa kusafiri njia inayotumiwa na maelfu ya wahamiaji haramu: kuvuka Jangwa la Sahara kisha Bahari ya Mediterania hadi Ulaya.
Francis Ngannou alivuka bahari hii ambayo imemeza vijana wengi wa Afrika, wakijaribu kuzifikia ndoto zao za maisha bora Ulaya. Lakini yeye alifanikiwa kufika Ulaya.
Kazi ya kupigana

Chanzo cha picha, Getty Images
Kufika Ufaransa, hakuacha wazo la kufanya mazoezi ya ndondi. Na kisha kuingia katika mashindano ya MMA na kufanikiwa kuwa bingwa.
Alifaulu kuonyesha ustadi wake wa mieleka wakati wa pambano dhidi ya Mfaransa Cyril Gane na kuubakisha mkanda wake wa ubingwa wa UFC wa uzito wa juu.
Licha ya mafanikio yake, baadaye aliamua kuondoka. "Unajua kwamba mkataba wa UFC unaweza kuwa na vikwazo na huna la kusema." Francis Ngannou alisema wakati anatoa tangazo la kuachana na UFC.
Baada ya kuondoka UFC, alifanikiwa kutia saini Ligi ya Wapiganaji (PFL), shirika jingine la MMA, ingawa ni la hadhi ya chini kuliko UFC.
Kushinda na kupoteza

Chanzo cha picha, Getty Images
2015, pambano lake la kwanza UFC: Francis Ngannou alipigana katika pambano lake la kwanza dhidi ya Mbrazili Luis Henrique baada ya kusaini UFC. Alishinda kwa kumpiga KO mpinzani wake katika raundi ya pili.
Kipigo cha kwanza akiwa UFC: Baada ya mfululizo wa ushindi, Francis Ngannou alipigana na Stipe Miocic aliyekuwa akitetea mkanda wake. Ngannou alipigwa katika pambano hilo.
Bingwa wa UFC uzito wa juu: Miaka mitatu baada ya pambano lao la kwanza, Miocic alitaka kutetea taji lake tena dhidi ya Mcameroon huyo. Francis Ngannou alifaulu kumshinda Miocic na kushikilia ukanda wa uzito wa juu.
Pambano lake dhidi ya UFC: Wakati Francis Ngannou alipotangaza kuondoka UFC, baadhi ya watu walishuku kwamba atarudi kwenye ulimwengu wa MMA. Hata hivyo, aliweza kuwanyamazisha baada ya kutia saini mkataba wa kihistoria na PFL.
Apata akitakacho

Chanzo cha picha, Getty Images
Akiwa na PFL, Francis Ngannou alipata uhuru aliokuwa ameutaka kutoka kwa UFC. Kuanzia sasa, ataweza kupigana kwenye ndondi - ndoto yake ya utotoni.
Pia atapata sehemu ya faida inayotokana na PFL kwenye hafla anazoshiriki. Mnyama huyo pia ameteuliwa kuwa balozi wa shirika hilo katika bara la Afrika.
Kwa mwandishi wa habari, Francis Ngannou ni nembo kwa vijana wa nchi yake.
"Francis ni kielelezo cha ustahimilivu, ni ishara ya ndoto iliyotimizwa kwa nguvu na mikono yake."
Oktoba 28, Francis Ngannou atatimiza ndoto yake ya utotoni. Anasaidiwa katika maandalizi na lejendari Mike Tyson ambaye pia atakuwa pembeni yake huko Riyadh.













