Kutana na James aliyeokoa maisha ya watoto milioni 2.4

Chanzo cha picha, Getty Images
Dunia inamsheherejea mmoja wa wachangiaji damu wenye rekodi duniani - ambaye plasma yake iliokoa maisha ya zaidi ya watoto milioni 2.4.
James Harrison alifariki katika nyumba ya wazee huko New South Wales, Australia tarehe 17 Februari, 2025, familia yake ilisema Jumatatu wiki hii. Amefariki akiwa na umri wa miaka 88.
Akijulikana nchini Australia kama "mtu mwenye mkono wa dhahabu," damu ya Harrison ilikuwa na kinga adimu, Anti-D, ambayo hutumiwa kutengeneza dawa anayopewa mama wajawazito ambao damu zao ziko hatarini kuwaathiri watoto wao ambao hawajazaliwa.
Shirika la Msalaba Mwekundu Australia, ambalo lilitoa heshima kwa Harrison, lilisema aliahidi kuwa mchangiaji damu baada ya kuchangiwa damu nyingi wakati akifanyiwa upasuaji mkubwa wa kifua akiwa na umri wa miaka 14.
Alianza kuchangia damu akiwa na umri wa miaka 18 na aliendelea kufanya hivyo kila baada ya wiki mbili hadi alipofikisha miaka 81.

Chanzo cha picha, Australian Red Cross Lifeblood
Mnamo 2005, aliweka rekodi ya dunia kwa kuchangia zaidi - rekodi aliyoshikilia hadi mwaka 2022 alipopitwa na mtu mmoja huko nchini Marekani.
Binti ya Harrison, Tracey Mellowship, alisema baba yake "alijivunia sana kuokoa maisha mengi, bila gharama au maumivu yoyote".
"Alisema kila wakati haiumizi, na maisha unayookoa yanaweza kuwa yako mwenyewe," alisema.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Mellowship na wajukuu wawili wa Harrison pia ni wapokeaji wa chanjo za anti-D.
"Ilimfurahisha [James] kusikia kuhusu familia nyingi kama yetu, ambazo zipo kwa sababu ya wema wake," alisema.
Chanjo za Anti-D huwalinda watoto ambao hawajazaliwa dhidi ya ugonjwa mbaya wa damu unaoitwa ugonjwa wa hemolytiki kwa mtoto mchanga, au HDFN.
Hali hii hutokea wakati wa ujauzito wakati seli nyekundu za damu za mama haziendani na zile za mtoto wake anayekua.
Mfumo wa kinga wa mama huona seli za damu za mtoto kama tishio na hutoa kinga za mwili kuzishambulia. Hii inaweza kumdhuru mtoto, na kusababisha upungufu mkubwa wa damu, kushindwa kwa moyo, au hata kifo.
Kabla ya hatua za anti-D kutengenezwa katikati ya miaka ya 1960, mtoto mmoja kati ya wawili waliogunduliwa na HDFN alifariki.
Haijulikani jinsi damu ya Harrison ilivyokuwa na kinga nyingi za anti-D, lakini ripoti zingine zilisema ilihusiana na kuongezewa damu kubwa aliyopokea akiwa na umri wa miaka 14.

Chanzo cha picha, Getty Images
Kuna wachangiaji wa anti-D wasiopungua 200 nchini Australia, lakini husaidia takriban mama 45,000 na watoto wao kila mwaka, kulingana na Huduma ya Damu ya Msalaba Mwekundu ya Australia, pia inajulikana kama Lifeblood.
Lifeblood imekuwa ikifanya kazi na Taasisi ya Utafiti wa Tiba ya Walter na Eliza Hall ya Australia kukuza kinga za mwili za anti-D kwenye maabara kwa kuiga seli za damu na kinga kutoka kwa Harrison na wachangiaji wengine.
Watafiti wanaohusika wanatumai anti-D iliyotengenezwa maabara inaweza siku moja kutumika kusaidia wanawake wajawazito ulimwenguni kote.
"Kutengeneza tiba mpya kwa muda mrefu imekuwa 'lengo muhimu'," mkurugenzi wa utafiti wa Lifeblood David Irving alisema.
Alibainisha uhaba wa wachangiaji waliojitolea kuchangia mara kwa mara, ambao wana uwezo wa kutoa kinga za mwili katika ubora na wingi wa kutosha.












