Iran ikiendelea kushambuliwa, Je, washirika wake Urusi na China wataingilia kati?

s

Chanzo cha picha, Anadolu via Getty Images

Muda wa kusoma: Dakika 6

Kwa kuwa Uingereza imeruhusu Washington kutumia kambi zake za anga kufanya mashambulizi ya "kinga" wakati wa vita vya Marekani na Israeli dhidi ya Iran, umakini umeelekezwa kwenye usaidizi ambao Tehran inaweza kupokea kutoka nje ya nchi.

Urusi na China zote zinaimarisha uhusiano imara wa kidiplomasia, kibiashara na kijeshi na Jamhuri hiyo ya Kiislamu, lakini mgogoro wa sasa utaamua ni kwa kiasi gani ziko tayari kuiunga mkono.

Urusi imeiunga mkono Iran kwa uwazi, lakini ni msaada ni mdogo

s

Chanzo cha picha, SPUTNIK/KREMLIN POOL/EPA/Shutterstock

Jibu la Moscow kwa mashambulizi ya pamoja ya Marekani na Israel dhidi ya Iran limekuwa kali lakini lenye mipaka, likionyesha hasira na mshikamano na Tehran, huku likiepuka kwa uangalifu hatua yoyote ambayo ingeiingiza Urusi moja kwa moja kwenye mzozo huo, kulingana na Sergei Goryashko, mwandishi wa habari wa BBC katika idhaa ya Urusi.

Msemaji wa Kremlin Dmitry Peskov alielezea "kukatishwa tamaa" kwamba, licha ya mazungumzo kati ya Washington na Tehran, hali hiyo "imezidi kuwa uchokozi wa moja kwa moja."

Aliongeza kuwa Moscow ilikuwa ikiwasiliana mara kwa mara na viongozi wa Iran na mataifa ya Ghuba yaliyoathiriwa na ongezeko hilo la mapigano.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Urusi ililaani kile ilichokiita "uchokozi usio na sababu" dhidi ya Iran uliofanywa na Marekani na Israeli na kulaani kile inachokiona kama mauaji ya kisiasa na "uwindaji" wa viongozi wa mataifa huru.

Siku ya Jumapili, Rais Vladimir Putin alitoa salamu zake za rambirambi kwa Rais wa Iran Masoud Pezeshkian kwa mauaji ya Kiongozi mkuu wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei, akiita kitendo hicho ni "ukiukwaji wa utu wa binadamu na sheria za kimataifa."

Hata hivyo, Kremlin imeepuka dhahiri kufanya ukosoaji wa kibinafsi dhidi ya Rais wa Marekani Donald Trump na inaendelea kueleza shukrani yake kwa juhudi za udhamini wa Marekani kuhusu Ukraine.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Alihojiwa Jumatatu juu ya Moscow sasa inavyoweza kuiamini Washington, Peskov alijibu kwamba Urusi "inaijiamini yenyewe zaidi ya yoyote" na alijitetea kulinda maslahi yake.

Maslahi haya yanaelezea kwanini msaada wa Urusi kwa Iran uko kwenye maneno zaidi kuliko vitendo, ingawa Tehran imekuwa mojawapo ya washirika wa karibu zaidi wa Moscow tangu uvamizi mkubwa nchini Ukraine, ikitoa ndege zisizo na rubani (drones) na kuwasaidia Urusi kubuni njia za kuepuka vikwazo vya Magharibi, anafafanua mwandishi wetu.

Iran pia inafaa katika taswira ya Kremlin ya utaratibu wa nguvu nyingi (multipolar), ambapo haki za mataifa zinawekwa mbele ya haki za binadamu na serikali zinadhibiti eneo lao kwa ukamilifu. Kuanguka kwa utawala kama huo kungepiga vita mfano huu kwa nguvu.

Wakati huo huo, Kremlin tayari imeonyesha zamani kwamba haitachukua hatari nyingi kwa ajili ya washirika wake, iwe huko Venezuela, Syria au wakati wa vita vya siku 12 kati ya Israel na Iran katika msimu wa joto wa 2025.

Mkataba wa ushirika wa kimkakati kati ya Urusi na Iran uliosainiwa Januari 17, 2025 si mkataba wa ulinzi wa pamoja.

Moscow na Tehran wameapa kushiriki taarifa, kufanya mazoezi ya pamoja, na "kulinda usalama wa kikanda," lakini hawajatangaza ahadi ya kuwalinda kwa kila mmoja endapo wangeushambulia.

Uhusiano wa kiuchumi kati ya nchi hizo mbili pia umedhoofika, na biashara kadhalika kati ya dola bilioni 4 na 5.

Hata hivyo, uhusiano wa kijeshi na viwanda unaimarika. Mnamo Februari, Financial Times ilitangaza makubaliano makubwa ambapo Urusi ingetoa kwa Iran mifumo ya ulinzi wa anga ya mkononi ya Verba yenye thamani ya euro milioni 500.

Iran imepokea ndege za mafunzo aina ya Yak-130, helikopta za kushambulia Mi-28 na inasubiri ndege za kivita Su-35, lakini Urusi bado haijatoa mifumo ya Verba.

Kwa Moscow, Iran ni muhimu sana kuiacha bila msaada, lakini sio muhimu vya kutosha kupigana kwa ajili yake. Uwiano huu unaweza kubadilika, lakini kwa sasa, ushiriki wa Urusi unaonekana kubaki kwa kauli zaidi.

Jukumu la China katika kunusuru uchumi

s

Chanzo cha picha, Iranian Ministry of Foreign Affairs/EPA/Shutterstock

China imekashifu vikali mauaji ya Ayatollah Ali Khamenei, huku Beijing ikiendelea kupinga mikakati ya Marekani ya kubadilisha utawala katika nchi mbalimbali duniani.

Kwenye msingi wa uhusiano kati ya China na Iran, kunapatikana ushirikiano wa kiuchumi, anaeleza Shawn Yuan wa Kitengo cha Global China cha BBC World Service.

China ndiyo mshirika mkubwa wa kibiashara wa Iran na mteja wake mkubwa wa nishati.

Licha ya vizuizi vikali vya Marekani dhidi ya Iran kwa miaka mingi, Beijing imeendelea kuwa mpiga debe wa uchumi wa Tehran, ikinunua mafuta kwa wingi kwa bei zilizopunguzwa kupitia mtandao wa "meli za giza," meli zilizoandikwa vibaya ili kuepuka vizuizi vya kibiashara.

Mfano ni mwaka 2025, ambapo China ilinunua zaidi ya 80% ya mafuta yaliyopelekwa na Iran, na mapato yaliyozalishwa na ununuzi wa China yaliwasaidia Iran kuimarisha uchumi wao na kufadhili matumizi ya ulinzi, hata wakati masoko ya Magharibi yalipofungwa.

Makubaliano ya kimkakati ya miaka 25 yaliyosainiwa mwaka 2021 yameimarisha uhusiano huu, yakiahidi uwekezaji wa mamia ya mabilioni ya dola za Marekani kutoka China katika miundombinu na teknolojia ya mawasiliano ya Iran.

"Mkakati wa muda mrefu" wa China

Kihistoria, China imekuwa ikichukua msimamo wa "kujizuia" na kutoa wito wa kupunguza mvutano kati ya Iran, Israel na Marekani.

Katika migogoro mbalimbali, China imekuwa ikipinga kile inachokiita "uingiliaji wa nje," kauli inayolenga zaidi sera za Marekani katika eneo hilo.

Wakati wa mapigano ya siku 12 kati ya Israel na Iran katika majira ya joto ya 2025, China ilisisitiza haja ya mazungumzo na utulivu.

Hata hivyo, haikuwahi kupendekeza kuingilia kijeshi moja kwa moja, bali ilijikita katika msimamo wa kidiplomasia.

Katika mizozo ya awali, China ilitumia nafasi yake katika baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kama kinga ya kisiasa kwa Iran.

Iliwahi kutumia au kutishia kutumia kura yake ya turufu kupunguza au kudhoofisha maazimio yaliyolenga kuishinikiza Tehran.

Mkakati wa Beijing umekuwa ni kuifanya Marekani ibaki ikijishughulisha na Mashariki ya Kati, bila kuruhusu hali kufikia kiwango cha kuanguka kabisa kwa eneo hilo. China ina maslahi ya kiuchumi, hasa katika nishati, hivyo haitaki machafuko makubwa yatakayopandisha bei ya mafuta duniani.

Kuibuka kwa utawala unaounga mkono Magharibi mjini Tehran kungekuwa pigo kubwa la kijiografia kwa China.

Iran ni mshirika muhimu wa kisiasa na kiuchumi, na pia ni mwanachama wa BRICS pamoja na Shanghai, jambo linaloimarisha ushawishi wa Beijing na Moscow.

Iwapo hakutakuwa na uvamizi mkubwa wa kijeshi dhidi ya Iran, kuna uwezekano miundo ya kisiasa na kijeshi ya nchi hiyo ikaendelea kuwepo.

China itaendelea kucheza "mchezo wa muda mrefu," tayari kushirikiana na yeyote atakayemrithi kiongozi Mkuu, huku Urusi nayo ikitafuta maslahi yake binafsi.