Je, ni maeneo gani ya Urusi yanayoweza kushambuliwa na makombora ya masafa marefu ya Marekani?

Chanzo cha picha, Getty Images
Maafisa wa Marekani wanasema Rais wa Marekani Joe Biden ameidhinisha Ukraine kutumia makombora ya masafa marefu yaliyotolewa na Marekani kushambulia nchini Urusi.
Hapo awali Marekani haikuruhusu, ikisema inaweza kuzidisha vita.
Mabadiliko makubwa ya kisera yanakuja miezi miwili tu kabla ya Joe Biden kukabidhi madaraka kwa Rais mteule Donald Trump.
Kuwasili kwa Donald Trump kumetilia shaka ya kuendelea kwa misaada ya Marekani kwa Ukraine katika siku zijazo.
Kwa nini Marekani ilitoa ruhusa kwa Ukraine?
Ukraine imekuwa ikitumia makombora haya ya masafa marefu (ATACMS) kwa zaidi ya mwaka mmoja kushambulia Urusi katika maeneo ya Ukraine yanayokaliwa na Urusi.
Makombora haya yanaitwa Army tactical missile system (ATACMS) kwa Kiingereza.
Lakini Marekani haijaipa Ukraine ruhusa ya kutumia makombora hayo ndani ya Urusi.
Makombora ya Lockheed Martin ndiyo silaha yenye nguvu zaidi iliyofikishwa Ukraine.
Ina uwezo wa hadi kufikia 300km sawa na maili 186 na ina uwezo wa kushambulia na kulenga adui.
Nchi hiyo iliishutumu kwa kuambiwa kauli kwamba ipigane ikiwa imefungwa mkono mmoja mgongoni mwake.
Kumekuwa na ripoti kuwa Marekani imebadili sera yake kufuatia kutumwa kwa wanajeshi wa Korea Kaskazini katika eneo la Kursk kwa ajili ya kuwaunga mkono wanajeshi wa Urusi.
Inafaa kukumbuka kuwa eneo hili la Urusi limekuwa chini ya udhibiti wa Ukraine tangu Agosti iliyopita.
Mashaka yamesalia kwa Marekani kuchukua msimamo mzuri zaidi kuelekea Ukraine baada ya Donald Trump kuchaguliwa tena kuwa rais.
Kwa sababu hii, inaonekana kwamba Biden, ambaye kwa sasa ndiye rais, ameamua kufanya awezalo kuisaidia Ukraine katika muda wake mfupi uliosalia kuwa madarakani.
Kwa kuimarisha jeshi la Ukraine, inaaminika kuwa kuna fursa kwa Ukraine kuwasilisha hoja yake kwa nguvu zaidi katika mazungumzo ya amani.

Chanzo cha picha, Shutterstock
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Ukraine inaweza kulenga ndani ya Urusi kwa kutumia kombora hili.
Ukraine inatarajiwa kuchukua hatua kwa lengo la kusalia eneo la Kursk kwanza.
Kwa sasa, jeshi la Ukraine lina udhibiti wa kilomita za mraba 1000 katika eneo hili.
Ukraine inatarajiwa kutumia makombora haya ya ATACMS kwa kujilinda, kushambulia na kulenga maeneo kama vile kambi za kijeshi za Urusi, miundo mbinu ya kijeshi na maghala ya silaha.
Makombora haya hayatatosha kubadilisha mkondo wa vita. Ikitarajia mabadiliko hayo ya sera, Urusi tayari imeweka vifaa vyake vya kijeshi, kama vile ndege za kivita, katika maeneo yake ya ndani.
Silaha hizi zinaweza kuipa Ukraine mazingira yenye mazuri kwani wanajeshi wa Urusi tayari wamesonga mbele katika eneo la mashariki.
"Hii sio mwisho kabisa," anasema balozi kutoka nchi za magharibi akiwa Kiev. Mwingine ambaye hakutaka kutambuliwa, alisema uamuzi huo umechukuliwa ili kuhakikisha uungwaji mkono kwa Ukraine.
Aliongeza kuwa hii inaweza kuongezea hasara Urusi vitani.
Evelyn Farkas, ambaye aliwahi kuwa naibu waziri wa ulinzi katika utawala wa Obama, alisema maswali kuhusu ni silaha ngapi zitatolewa pia sasa yanaibuliwa.
"Kuna swali la ni makombora mangapi wanayo. Wizara ya Ulinzi ya Marekani imeonya kwamba hawana makombora ya kutosha kuipatia Ukraine ," aliongeza.
"Kutumia kombora hili la ATACMS kulenga maeneo kama vile daraja la Kerch linalounganisha Urusi na Crimea kunaweza kuwa na athari chanya ya kisaikolojia kwa Ukraine," Farkas alisema.
Uidhinishaji huu wa Marekani unatarajiwa kusababisha kuidhinishwa kwa matumizi mengine ya silaha. Kwa mfano, Uingereza na Ufaransa zinaweza kuruhusu makombora ya Storm Shadow kutumiwa ndani ya Urusi.
Makombora haya yana sifa zinazofanana na za makombora ya ATACMS ya Marekani. Makombora ya Storm Shadow yanatengenezwa kwa pamoja na Ufaransa na Uingereza.

Chanzo cha picha, Getty Images
Je, hatua hii itazidisha vita katika eneo hilo?
Utawala wa Biden hadi sasa umekataa kuruhusu Ukraine kutumia makombora haya, ikihofia kwamba vita vinaweza kuongezeka.
Rais wa Urusi Putin alipotaja suala hili, alionya kwamba nchi za NATO zinaweza kufikiriwa kwamba zinashiriki moja kwa moja katika vita ikiwa silaha za Magharibi zitatumika kushambulia ardhi ya Urusi.
Bila shaka hii inaweza kubadilisha hali ya vita, Putin alisema mnamo Septemba. "Ina maana kwamba nchi za NATO, Marekani na nchi za Ulaya zinapigana dhidi ya Urusi," alisema.
Urusi tayari imepinga usambazaji wa vifaru vya kisasa na ndege za kivita kwa Ukraine, ikisema itakuwa ikivuka mstari mwekundu'. Hatahivyo, msaada wa kijeshi wa NATO kwa Ukraine unaendelea bila kuchochea moja kwa moja vita na Urusi.
Aliyekuwa balozi wa Marekani katika muungano wa NATO, Kurt Voelker, alisema, "Marekani imefanya maamuzi ya kiholela na yasiyo ya haki juu ya ulinzi wa Ukraine kwa kuweka masharti kwamba Ukraine haipaswi kutumia silaha za Marekani."
Pia alikosoa kwamba "uamuzi wa kutumia makombora ya ATACMS yenye vizuizi haukuwa mzuri. Ulichukuliwa kwa hofu kwamba huenda ukaichokoza zaidi Urusi."
"Kwa wakati huu, itakuwa vibaya kufanya uamuzi huu wa sera hadharani kwa sababu ungeruhusu Urusi kujiweka tayari," alisema.

Chanzo cha picha, Shutterstock
Trump atafanya nini atakapoanza majukumu ya urais?
Donald Trump amebakiza miezi miwili kushika hatamu za Ikulu ya White House.
Tayari, Ukraine imeeleza nia yake ya kumaliza vita. Anaweza kukataa kutumia makombora haya baada ya kurejea madarakani.
Wengi wa washirika wa Donald Trump wamekosoa hatua hiyo, bila tangazo rasmi la ikiwa ataendeleza sera hiyo.
Mtoto wa Trump, Trump Jr, alichapisha maoni yake kwenye mtandao wa kijamii akisema, "Wazalishaji wa silaha za kijeshi wanajaribu kuanzisha Vita vya Tatu vya Dunia kabla ya baba yangu kurejea mamlakani na kuokoa watu."
JD Vance, ambaye amechaguliwa kuwa makamu wa rais, amesema kuwa Marekani haipaswi kutoa msaada wa kijeshi kwa Ukraine.
Lakini wanachama wengine wa utawala wake wana maoni tofauti. Michael Waltz, mshauri wa usalama wa taifa katika utawala wa Trump, amesema kuwa uwasilishaji wa silaha mara moja kwa Ukraine unapaswa kuisaidia Urusi kuilazimisha Ukraine kuingia katika mazungumzo ya amani.
Haijabainika ni uamuzi gani Donald Trump atafanya. Hata hivyo, wengi wanahofia kwamba baada ya kuingia madarakani, upelekaji wa silaha nyingi kwa Ukraine, ikiwa ni pamoja na ATACMS, utasitishwa.
"Inatutia wasiwasi. Tunatumai kuwa Trump hatabadilisha sera hii," mjumbe wa bunge la Ukraine Oleksiy Koncharenko aliambia BBC.
Imetafsiriwa na Martha Saranga na kuhaririwa na Seif












