Waridi wa BBC: Wanaharakati wa masuala ya wanawake wanapaswa kuheshimu haki za wanaume

Mama Mongela

Chanzo cha picha, Mama Mongela

    • Author, Na Martha Saranga
    • Nafasi, BBC Swahili, Dar es Salaam
  • Muda wa kusoma: Dakika 4

Mimi nililelewa katika familia ambayo wazazi walipendana sana na niliwaona wakipendana.

Sikulelewa katika familia ya magomvi.

Gertrude Mongela anasema hali hiyo ilimpa amani sana, hakuwa mwoga wala na hofu.

"Baba alikuwa muelewa, alitulea kwa upendo sana. Alikuwa anakagua madaftari na mitihani na kunisifia kila nilipofanya vizuri.

‘’Nilipozaliwa Septemba 13, 1945 baba yangu alinipa jina la Getrude akitaka niwe na nguvu kama mkuki’’anaeleza.

‘’Kuna mambo yalikuwa yanafanywa dhidi ya wanawake utadhani wanawake ni raia namba mbili ulimwenguni’’

Jamii iliwaona wanawake kama watu wasio na uwezo, iliwaweka chini ya wanaume katika mambo mengi sana, mfano hawakuwa wakipiga kura kuchagua viongozi, wala hawakuwa viongozi.

Ndivyo anavyoanza simulizi Balozi Gertrude Mongela mzaliwa wa kisiwa cha Ukerewe kinachopatikana kilizopo ziwa Victoria nchini Tanzania.

Ndoto yake ya kuwa mwalimu na hatimaye kiongozi iling'ara baada ya kuhitimu masomo ya ualimu katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam 1970.

Anakumbuka mara kadhaa alimsikia mwalimu mkuu akitoa maelekezo shuleni na kusema "haya ni maagizo kutoka juu" ikimaanisha yatekelezwe.

Alijihoji huko juu ni wapi? nilitamani sana kujua huko juu ambako kuna maagizo kila mara kuna nini hata nisifike?

"Nikaazimia moyoni mwangu kwamba hao walioko juu wakitoa maagizo tu ni binadamu kama mimi, natamani kufika huko"

Baba alinisimulia kuwa Gertrude ni jina lenye asili ya Ujerumani lililomaanisha mtu mwenye nguvu kama mkuki..ndivyo baba yangu alivyonikusudia, anaeleza Bi Gertrude akitabasamu.

"Hata mama yangu,alikuwa hodari sana, hakuwa mwanamke wa kuchezea, mama yangu alikuwa anajiamini sana, alikuwa na msemo wake kwamba hapa duniani unaweza kuumba chochote kwa mikono yako isipokuwa mtoto”.

Ilikuwaje kuwa mwenyekiti wa kongamano la nne la kimataifa la wanawake la Beijing, China 1995?

"Hakika ni mwenyezi Mungu alinipa uwezo na kibali hicho"anaeleza Bi Mongela

Mbali ya malezi ya nyumbani anasema maisha yake yote ya elimu alilelewa katika shule za imani ya madhehebu ya Katoliki ambazo falsafa yake ni ujasiri na uthubutu ilimjenga kuwa mwanamke jasiri mwenye kuthubutu.

Anasema tangu wakati huo aliamini wanawake na wanaume wote kwa pamoja wana uwezo wa kujenga mataifa yao popote duniani.

Hakuna kiumbe mualikwa duniani kwa kuwa sote tumeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Wanawake wasinyanyase wanaume, na wanaume wasiwanyanyase wanawake.

Nguvu, maazimio na malengo ya mkutano wa Beijing yanafanikiwa leo?

Mama Mongela

Chanzo cha picha, Mama Mongela

Anasema anafarijika sana kuona mabadiliko makubwa katika jamii kote duniani, kwani dunia imetoka mbali sana.

‘’Leo ninapoona idadi kubwa ya watoto wa kike wakiandikishwa shule,wakifaulu vizuri na kufanya mambo mbalimbali ambayo hapo kitambo haikuwezekana au walifanya kwa uchache inanifariji sana”, anaelezea Bi Getrude Mongela.

Harakati na uongozi wa kisiasa na malezi ya familia

Mama Mongela akila kiapo

Chanzo cha picha, Mama Mongela

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Mama Beijing Gertrude Mongela kama baadhi ya watu walivyomuita, aligonga vichwa vya habari ndani na nje ya Afrika wakati huo akiwa mwenyekiti wa kongamano la nne la wanawake la Umoja wa Mataifa 1995.

‘’Niliona nina kipaji na akili nyingi, jambo ambalo hata watu walionizunguka walikuwa wakiniambia, nikawa ninajiambia ninaweza kufanya lolote’’

Mwaka 2000 hadi 2010 alipata ridhaa ya wananchi na kuwa mbunge wa jimbo la Ukerewe kwa vipindi viwili.

Haikuwa rahisi lakini anasema alijitahidi kutekeleza majukumu yake vizuri kuthibitisha ukweli kwamba wanawake wanaweza kufanya vizuri kama wanaume.

Wakati wote huo tayari alikuwa amekwishafunga ndoa na mume wake Silvin Mongela.

,katika harakati za kazi ndipo alipokutana na Silvin Mongela ambaye akawa mume wake waliyedumu kwa miaka 55 sasa.

Bi Mongela anasema amejaaliwa kupata watoto watatu wote wa kiume.

"Ni muhimu sana hata kwa waanaharakati wa masuala ya wanawake kuheshimu haki za wanaume wakati unapigania za wanawake "Anaeleza kuwa mume wake wakati wote amekuwa msaada na nguzo yake.

Anasema mara nyingi mume alibaki na watoto wao wakati yeye akitimiza majukumu mbalimbali ikiwemo safari na mikutano ya mbali.

Anajivunia kuwa mama Beijing, kuona sauti walizopaza zikizaa matunda. Anakumbuka namna alivyosafiri mataifa ya mbali na kukutana na ubaguzi wa rangi wa waziwazi.

Anasema haikumbabaisha aliwatazama usoni na kuwaambia kuwa si jambo la kiungwana.

Nyakati gani adhimu anazozikumbuka na kumpa furaha?

Mama Mongela

Chanzo cha picha, Mama Mongela

Nimetembea sehemu nyingi na kukutana na watu wengi duniani, kwa uchache tu nitakueleza kuhusu Mandela, Fidel Castro na Papa Yohane Paulo wa pili.

Anafafanua: Mandela nilikutana naye mara nyingi kwa sababu ya mke wake, Graca Machel alikuwa rafiki yangu. Mwaka 2010 nilikwenda kumtembelea Nelson Mandela Afrika Kusini, Graça Machel mke wake alikuwa rafiki yangu sana.

‘’Nakumbuka nyakati ambazo tulicheka sana nikimuuliza vipi rafiki yangu hivi wewe unaangukia tu kwa marais? anaeleza Bi Mongela huku akishindwa kuzuia kicheko.

”Unajua kilichonifurahisha kwa Mandela kubwa zaidi ni namna alivyokuwa anaendesha magereza yake.Wafungwa walifunguliwa akaunti ambapo wakiwa gerezani walikuwa wakifanya kazi na kulipwa, siku akitoka gerezani anapewa ujira wake kama mtaji asije akafanya maovu.

Kuhusu aliyekuwa Rais wa Cuba anasema: Fidel Castro wa Cuba nilifurahi sana kukutana naye, nilipenda sera na namna alivyokuwa anaendesha nchi yake.

”Papa Yohane Paulo wa pili nimekutana naye mara nne, sijasahau mara ya mwisho wasaidizi wake walipotaka kunitambulisha kwake alisema, ‘’This is Gertrude, I know her’’ (Huyu ni Gertrude ninamfahamu) nilijiskia furaha sana.

”Ninajiskia vizuri kukutana na watu wengi sana waliojenga nchi hii. Kina mama Leah Lupembe, Thabit Kombo na wengine wengi tuliohudumu pamoja katika Chama cha Mapinduzi na serikali”.

Anasema: Ninajiskia fahari sana ninapokutana na wanawake wa mijini na vijijini kwa mfano nyumbani kwetu Ukerewe ambao walipokea mabadiliko na kuleta mchango chanya kwenye jamii yetu.

Jambo gani watu hawalifahamu kukuhusu?

”Ninajua kupika, najua kucheza muziki, lakini mara zote nilikuwa ninacheza na mume wangu, kuimba tu sijui.

Nilijitahidi sana kulea watoto wangu vema lakini sijui kama nimefanikiwa kurithisha nyayo zangu, hilo jamii inaweza kueleza lakini ninajivunia mjukuu wangu mmoja ninamuona akiishi nyayo zangu kabisa, ni mwanamke jasiri hasa anayepigania ndoto zake.

Imehaririwa na Florian Kaijage