Wajue viongozi walioanza kazi katika burudani na michezo kabla ya kuingia Ikulu

- Author, Rashid Abdallah
- Nafasi, Mchambuzi, Tanzania
George Weah (55) rais wa sasa wa taifa la Magharibi mwa Afrika, Liberia. Aliingia madarakani Januari 2018 chini ya chama cha Congress for Democratic Change.baada ya kujikingia ushindi wa asilimai 61.5.
Weah alirithi kiti cha urais kutoka kwa mwanamke wa kwanza kuchaguliwa kuwa rais barani Afrika, Ellen Johnson Sirleaf. Kabla ya kuingia katika kinyanganyiro cha urais, Weah alikuwa seneta katika Bunge la Liberia.
Ndiye mchezaji mpira wa kwanza barani Afrika kuwa rais wa nchi. Kwa miaka 14 amecheza mpira katika mataifa ya Ulaya; Ufaransa, Italy na Uingereza akichezea vilabu vikubwa vya soka kama Monaco, Paris Saint-Germain, AC Milan, Chelsea, Manchester City na Marseille.
Mchezaji wa zamani wa mpira wa magongo, Mmarekeni, Sparky Anderson, katika nukuu yake maarufu anasema, "unaweza kuwa yeyote unayetaka kuwa, muhimu uweke jitihada za kutosha."
Ulimwengu umezoea kuwaona wanasiasa wakitoka katika familia za wanasiasa, ama wanasiasa waliojiekeza katika elimu au hata wafanyabiashara wakubwa wanaotumia pesa zao kuingia katika siasa.
Lakini wapo wanasiasa ambao maisha yao hadi kufikia katika siasa na kuwa watawala, walianza katika kazi ambazo hazina mwelekeo kabisa wa kisiasa. Orodha ya viongozi wa nchi ambao walianza kazi katika michezo na burudani kabla kuingia Ikulu:
Volodymyr Zelenskyy, Rais wa Ukraine, Mchekeshaji

Aliingia madarakani Mei 2019, ni rais wa sita wa Ukraine.
Nchi yake kwa sasa inakumbana na mtihani mkubwa baada ya kuvamiwa na Urusi. Mamia ya watu wameshauawa na maelfu wameikimbia nchi.
Licha ya Rais Zelenskyy kukosa mizizi katika siasa na utawala, ameonesha uwezo mkubwa wa kiuongozi wakati huu wa vita. Ameonesha ukomavu mkubwa. Kutoka mchekeshaji hadi shujaa wa taifa.
Kabla ya kuwa Rais, alijipatia umaarufu mkubwa kwa kazi ya uchekeshaji katika majukwaa ya sinema na mfululizo wa filamu fupifupi za kuchekesha zilizopewa jina la "Mtumishi wa Watu".
Kwa sasa ana umri wa miaka 44, alianza shughuli za uigizaji na uchekeshaji akiwa na miaka 17. Mwaka 2015 ndipo msururu wa vichekesho vya Mtumishi wa Watu vilipoanza kupeperushwa katika televisheni, akiigiza kama Rais wa Ukraine.
Jacinda Ardern, Waziri Mkuu wa New Zealand, DJ wa muziki

Jacinda Ardern ni Waziri Mkuu wa 40 wa New Zealand, kutoka chama cha Labour. Aliingia madarakani 2017, kabla ya hapo alihudumu katika kiti cha Ubunge baada ya kushinda uchaguzi mkuu wa 2008.
Wakati anaingia madarakani alikuwa kiongozi mdogo zaidi kiumri kuongoza serikali, wakati huo akiwa na miaka 37. Katika uchaguzi mkuu wa 2020 chama chake kilijipatia ushindi mkubwa, ambao ulitokana na kukuwa kwa ushawishi wa Waziri Mkuu huyo.
Alianza kukubalika nje ya nchi kwa kuwa kiongozi mwenye umri mdogo. Pia, namna alivyo shughulikia mashambulio katika misikiti miwili katika mji wa Christchurch, yaliyouwa watu 49, kulimpa umaarufu mkubwa nje ya nchi yake.
Mapambano dhidi ya Uviko 19 ni karata muhimu iliyompa ushawishi mkubwa New Zealand. Nchi hiyo imefanikiwa kudhibiti maambukizo kuwa chini, na kuwa mfano katika ulimwengu wa nchi iliyofanikiwa katika mapambano dhidi ya ugonjwa huo.
Kabla ya kuwa Waziri Mkuu na kuwa Mbunge, Jacinda Ardern alipata kuwa DJ wa muziki katika matamasha na vilabu vya burudani nchini New Zealand. Katika ukurasa wake wa Instagram bado zipo picha akiwa DJ na jumbe za zamani akihamasisha watu kuhudhuria matamasha hayo.
Imran Khan, Waziri Mkuu wa Pakistan, mchezaji kriketi

Imran Khan, Waziri Mkuu wa sasa wa Pakistan, na kiongozi mkuu wa serikali. Ni Waziri Mkuu wa 22 katika taifa la wakaazi milioni 220 na lenye silaha za nyuklia. Khan aliingia madarakani August 2018.
Kabla ya kuwa Waziri Mkuu, hakuwa mgeni wa siasa za Pakistan. Ingawa kilichompa umaarufu zaidi ni kuwa mchezaji wa kimataifa wa kriketi. Alikuwa kapteni wa timu ya taifa ya Pakistan iliposhinda kombe la dunia la kriketi mwaka 1992.
Imran Khan (69) yuko katika mtihani mkubwa wakati huu, juu ya hatima ya uongozi wake. Nchi hiyo inakabiliwa na mfumuko mkubwa wa bei, akilaumiwa kwa usimamizi mbaya wa uchumi. Sauti kadhaa za wapinzani wake kisiasa zinasikika kila uchao zikimtaka ajiuzulu.
Andry Rajoelina, Rais wa Madagascar, DJ wa muziki

Andry Rajoelina ni rais wa sasa wa kisiwa cha Madagascar katika bahari ya Hindi. Aliapishwa Januari 2019. Awali alikuwa rais wa mpito kutoka 2009 hadi 2014 baada kukimbia nchi aliyekuwa rais wa taifa hilo Marc Ravalomanana mwaka 2009.
Vuguvugu la upinzani likiongozwa na Rojoelina, lilimfanya Ravalomanana kukimbilia Afrika ya Kusini. Umoja wa Afrika ulieleza kilichotokea Madagascar ni mapinduzi. Na kupelekea, wafadhili wa kimataifa ikiwemo Marekani kuzuia msaada wa kifedha wa mamilioni kwa taifa hilo.
Kabla ya kuingia katika ulingo wa kisiasa, Rojoelina alikuwa mfanyabiashara katika kampuni ya uchapishaji na matangazo. Akiwa na miaka 20 alikuwa DJ wa muziki katika vilabu vya usiku na mabaa katika mji wa mkuu wa Madagascar, Antananarivo.
Wapo pia viongozi walioanza shughuli za maisha katika uchekeshaji na wameondoka madarakani hivi karibuni: Marjan Sarec, aliyekuwa Waziri mkuu na ndiye mkuu wa Serikali ya taifa la Ulaya ya kati, Sloveni kutoka 2018 hadi 2020.
Jimmy Morales, alikuwa rais wa 50 wa taifa la Amerika ya Kati la Guatemala. Alihudumu katika nafasi hiyo kutoka 2016 hadi 2020. Kabla ya kuingia katika siasa na kuwa rais, bwana Morales alikuwa mchekeshaji katika televisheni.













