'Mimi ni mpambanaji, Mimi ni mtoto wa ghetto' - Eddy Kenzo

Kwa mtu ambaye ameishi muda mwingi mtaani , Eddy Kenzo ambaye ni mwanamuziki wa Uganda anaweza kuonekana kuwa mtu mwenye tabia ya kushangaza katika maisha.
Kenzo anasema yeye yupo ili kuhamasisha hisia nzuri, anataka kuwaonesha watu aina gani ya maisha ambayo watu wanapitia.
"kuna upande mwingine wa furaha, na sio simulizi za simanzi tu kila wakati" asema Kenzo.
Mama yake Kenzo alifariki wakati yeye akiwa na umri wa miaka mitatu tu. Hivyo miaka 13 iliyofuata baada ya kifo cha mama yake , yeye na kaka yake waliishi mtaani.
"Kitu pekee ambacho nilikifanya ni kutafuta kitu cha kula. Nilikuwa naenda sehemu ambayo nitaosha vyombo au kusaidia watu kwa namna mbalimbali katika kituo cha daladala. Nikawa mbeba mizigo katika majengo mbalimbali. Maisha yalikuwa hivyo tu."
Kama vijana wengine wengi, Kenzo alikuwa na ndoto ya kuwa mwana soka. Lakini hisia zake za kupenda burudisha watu zilimpeleka katika muelekeo tofauti.
"Nilikuwa naimba, nachezea watu - nilipenda muziki sana wakati nnaishi mtaani. Nilikuwa nawaburudisha watu na walikuwa wanafurahi mara zote."

Chanzo cha picha, Emma Tickson
Mwanamuziki huyo mwenye miaka 30-hana wasiwasi tena kuhusu suala la kupata mlo mmoja kwa siku.
Ni mwanamuziki nyota Uganda na Afrika Kwa ujumla na nyimbo zake zinajulikana duniani kote.
Hivi karibuni alionekana kwenye tangazo la makutano ya Times Square mjini New York linalotangaza wimbo wake mpya.
Ni wimbo wake mpya wa Missounwa, akiwa na mwanamuziki mkongwe wa Ivory coast Monique Séka uliorekodiwa wakati wa marufuku ya usafiri kutokana na mlipuko wa corona, ambapo Kenzo alikwama Ivory coast kwa kipindi cha miezi mitano.
"Nilijaribu kufanya kitu ambacho kingefanya akili yangu isifikirie uoga niliokuwa nao kuhusu corona, wakati nilipokuwa ndani bila kujihusisha na watu wengine."
Kutoka kwenye maisha ya mtaani mpaka maisha ya kujifungia ndani kwa miezi mitano kutokana na corona, mambo mengi yamebadilika sana kwa Eddy Kenzo.
Lakini anasema maisha yake ya kukua katika mazingira magumu yatabaki maishani mwake milele.
"Mimi ni mpambanaji, Mimi ni mtoto wa ghetto," Kenzo aliiambia BBC.
Aliongeza kusema kuwa ilikuwa ndoto yake kuwa na mashabiki na kuwa mnyenyekevu tangu mwanzo ili kuwa mkubwa kila siku. Hayo ndio maombi yake kila siku.












