Balozi wa Iran atilia shaka 'umuhimu wa mazungumzo' na Marekani
Chanzo cha picha, EPA
Balozi wa Iran katika Umoja wa Mataifa mjini Geneva, Ali
Bahreini, ametilia shaka uwezekano wa mazungumzo na Marekani.
"Kwa sasa tuna shaka sana kuhusu umuhimu wa
mazungumzo," Ali Bahreini aliwaambia waandishi wa habari mjini Geneva siku
ya Jumanne, kulingana na shirika la habari la Reuters.
Hili linawadia baada ya Rais wa Marekani Trump kutangaza
kuwa mazungumzo "yamechelewa sana" katika chapisho lake
kwenye jukwaa lake la Truth Social.
Shirika la misaada ya kibinadamu lasema idadi ya vifo nchini Iran yafikia 787
Takriban watu 787 wameuawa nchini Iran tangu Marekani na
Israel zilipoanzisha mashambulizi nchini humo Jumamosi, shirika la msalaba
mwekundu nchini Iran linasema.
Wakati huo huo, wanaharakati wa kutetea haki za binadamu
nchini Iran (HRANA) wenye makao nchini Marekani wanaripoti kwamba raia 742
wamekufa, wakiwemo watoto 176.
Fatemeh Mohammadbeigi, mjumbe wa tume ya afya ya bunge la
Iran, alisema Jumatatu kwamba hospitali tisa zililengwa nchini Iran,
akiishutumu Israeli na Marekani kwa kuzilenga.
Jeshi la IDF limejibu madai ya kulenga Hospitali ya Gandhi
huko Tehran, likisema shambulio hilo "halikulengwa hospitalini".
Wizara ya mambo ya kigeni ya Iran leo imeishutumu Israeli na
Marekani kwa kulenga hospitali hiyo.
Rais wa
Marekani Donald Trump anasema uongozi wa kijeshi wa Iran "umesambaratika"
na kwamba "ni kuchelewa" kufanya mazungumzo na Iran, katika chapisho
fupi aliloweka kwenye akaunti yake ya Truth Social.
"Ulinzi
wao wa anga, Jeshi la Anga, Jeshi la Wanamaji, na Uongozi umesambaratika.
Wanataka tuzungumze. Nimesema 'ni Kuchelewa Sana!'," ameandika rais,
akijibu makala ya Washington Post iliyompongeza kwa uamuzi wake wa kushambulia
Iran.
Siku ya
Jumapili, Trump alisema "angezungumza" na viongozi wa Iran kama
wangetoa ombi la kutaka kufanya hivyo, hata alipoendelea na mashambulizi yake na
Israeli na kuwasihi Wairani kuiangusha serikali hiyo.
Trump asema 'inasikitisha kuona' uhusiano wa Marekani na Uingereza ukisambaratika kwa mashambulizi ya Iran
Chanzo cha picha, Reuters
Rais Donald
Trump amemkosoa Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer kwa mara ya pili wiki
hii, akisema "inasikitisha kuona" uhusiano wa kipekee ukiharibika
baada ya Uingereza kusita kutoa msaada kwa mashambulizi ya Marekani dhidi ya
Iran.
Starmer amesema
Uingereza haikushiriki katika shambulizi dhidi ya Iran lililofanywa na Marekani
na Israeli kwa sababu hatua yoyote ya kijeshi ya Uingereza lazima iwe na
"mpango unaofaa uliotathminiwa vyema" na hakuamini katika "kupinduliwa
kwa serikali kupitia nguvu ya nje".
Lakini tangu
wakati huo ameruhusu Marekani kutumia kambi za Uingereza kuanzisha kile
alichokiita mashambulizi kidogo ya kujilinda ili kudhoofisha uwezo wa
Iran, ambayo imewashambulia washirika wa Marekani katika eneo hilo kwa ndege
zisizo na rubani na makombora.
Siku ya
Jumatatu, kambi ya Uingereza huko Cyprus ilishambuliwa na ndege isiyo
na rubani ambayo maafisa wa Cyprus walisema huenda ilirushwa na kundi la
Hezbollah la Lebanon linaloungwa mkono na Iran.
Trump
alisema hakuhitaji msaada wa Uingereza kuishambulia Iran lakini akaongeza kuwa
kusuasua huko kumeikatisha tamaa.
"Inasikitisha
sana kuona kwamba uhusiano huu si kama ulivyokuwa," Trump aliambia gazeti
la Sun katika mahojiano yaliyochapishwa Jumanne.
Aliambia
Telegraph siku ya Jumatatu kwamba Starmer alionekana kuwa na "wasiwasi
kuhusu uhalali" wa mashambulizi dhidi ya Iran, alipoanza kufikiria iwapo ataruhusu
kambi muhimu ya kijeshi ya Uingereza, Diego Garcia, itumike.
Akizungumza
na gazeti la Sun, Trump alisema kwamba hajawahi kufikiria kuwa angeiona
Uingereza ikiwa mshirika wa kusuasua, na badala yake alizisifu Ufaransa na
Ujerumani.
"Huu
ulikuwa uhusiano imara zaidi kuliko wote," alisema. "Na sasa tuna
uhusiano imara sana na nchi zingine barani Ulaya."
"Ufaransa
imekuwa bora. Wote wamekuwa wazuri. Uingereza imekuwa tofauti sana na nchi zingine."
Uingereza,
Ufaransa na Ujerumani zote zilitoa taarifa ya pamoja kujibu mashambulizi
ya Iran siku ya Jumamosi, zikisema kwamba zilikuwa na mawasiliano ya
karibu na Marekani, Israel na washirika wake katika eneo hilo, na zikatoa wito
wa kuanza tena kwa mazungumzo.
Starmer
amekosolewa kutoka pande zote za nyumbani kwa uamuzi huo, huku wapinzani upande
wa kushoto wakimtaka alaani kitendo hicho cha kijeshi na upande wa kulia,
viongozi wa upinzani Kemi Badenoch na Nigel Farage wakimshambulia Starmer kwa
kushindwa kumuunga mkono mshirika mkuu wa usalama na ujasusi wa Uingereza.
Wanajeshi wa
Pakistan na Afghanistan wamekabiliana katika sehemu nyingi kando ya mpaka wao leo
siku ya Jumanne huku ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Afghanistan ukionya
kwamba raia 42 nchini humo wameuawa hadi kufikia sasa katika mzozo huo wa siku
sita.
Mataifa hayo
ya Asia Kusini yaliogeuka kuwa maadui yamehusika katika mapigano yao
mabaya zaidi kuwahi kutokea katika miaka kadhaa kufuatia mashambulizi ya anga
ya Pakistani kwenye miji mikubwa ya Afghanistan wiki iliyopita, na kuzua hofu
ya mzozo mwingine wa muda mrefu katika eneo hilo ambalo pia linakabiliana
na mashambulizi ya Marekani na Israel dhidi ya Iran.
Pakistan imerusha
makombora ya angani hadi ardhini katika maeneo ya kijeshi ya Taliban katika
wiki iliyopita, na hata kuilenga moja kwa moja serikali ya Taliban katika
mashambulizi yasiyo ya kawaida kwa madai kwamba inawahifadhi wanamgambo
wanaotekeleza mashambulizi dhidi ya Pakistan kutoka nchini mwake. Hata hivyo, Taliban
imekanusha kusaidia makundi ya wanamgambo.
Waziri wa
Habari wa Pakistani Attaullah Tarar alisema Jumanne kwamba mashambulizi ya anga
yaliyofanikiwa yalifanyika kwenye kambi ya anga ya Bagram kaskazini mwa Kabul,
ambayo ilitumika kama kituo muhimu cha amri cha Marekani katika vita vya
Afghanistan vya miaka 20.
"Tulikuwa
na taarifa za kijasusi kwamba kulikuwa na silaha na vifaa muhimu vinavyotumiwa
na magaidi kupigana na jeshi la Pakistan kando ya mpaka na pia na wanajeshi wa
Taliban wa Afghanistan," Tarar aliambia Reuters katika taarifa rasmi ya
kwanza ya Pakistan kuhusu mashambulizi hayo.
Chanzo kikuu
cha usalama cha Pakistan kilisema mashambulizi ya angani yataendelea hadi
Afghanistan itakapochukua hatua madhubuti za kukabiliana na wanamgambo
wanaotumia eneo lake.
Ikiwa hatua
kama hizo hazitachukuliwa, Pakistan inaweza kulenga uongozi mkuu wa Taliban,
chanzo hicho kilisema.
Marekani lazima ishirikiane na upinzani ndani ya Iran - mshauri wa zamani wa Trump
Chanzo cha picha, Getty Images
Awali, John
Bolton, mshauri wa usalama wa taifa wa Donald Trump wakati wa muhula wake wa
kwanza kama rais, aliambia BBC World Service kwamba ni "muhimu" kwa
Marekani kushirikiana na upinzani ndani ya Iran.
Hakuna mtu
anayeweza kuwapa watu wa Iran "uhuru kwa urahisi", "itabidi
wasaidie kuupata", alisema.
Bolton aliongeza
kuwa hii inapaswa kuhusisha kutambua majenerali ambao "huenda wakawa
upande wao", pamoja na kuwapa wapinzani rasilimali na uwezo wa
mawasiliano.
"Swali ni
ikiwa Rais Trump ana uvumilivu na uthabiti wa kufanikisha jambo hili,"
Bolton aliongeza.
Vita kati ya Marekani na Israel dhidi ya Iran: Vifo vyafikia 787
Chanzo cha picha, AFP/bbc
Taarifa za hivi punde kutoka Shirika la Red Crescent la Iran zinaonyesha kwamba idadi ya vifo kutokana na mashambulizi ya pamoja ya Marekani na Israel dhidi ya Iran imeripoti kufikia takriban watu 787 watu.
Taarifa zinasema wengi wa waliopoteza maisha ni raia, huku mapigano yakiendelea na uhasama wa kijeshi ukizidi kupanuka katika Mashariki ya Kati.
Israel na Marekani zinaendelea kushambulia maeneo mbalimbali nchini Iran, na Iran ikiendelea kujibu mashambulizi hayo kwa makombora na ndege zisizo na rubani katika maeneo yanayohusiana na maslahi ya Marekani na Israel, zikiwemo kambi za jeshi katika nchi jirani
Hali bado ni tete na taarifa za vifo zinaendelea kubadilika kadri mapigano yanavyoendelea. Mapema Israel ilishambulia ofisi za rais wa Iran mjini Tehran.
Habari za hivi punde, Jeshi la Israel lasema limeshambulia ofisi ya rais ya Iran
Chanzo cha picha, Telegram/VahidOnline
Taarifa mpya
kutoka jeshi la Israeli zinasema jeshi lake la anga limeshambulia eneo la
uongozi wa utawala wa Iran.
Katika
taarifa kwenye mtandao wa Telegram, IDF inasema "silaha nyingi" zimeelekezwa
kwenye Ofisi ya Rais na Baraza Kuu la Usalama wa Kitaifa.
Inaongeza
kwamba taasisi ya mafunzo ya kijeshi na "miundombinu muhimu ya ziada ya
utawala" pia iliathiriwa.
Kiongozi
Mkuu wa zamani wa Iran Ayatollah Ali Khamenei alitumia eneo hilo, IDF inasema.
Khamenei
aliuawa katika eneo lake mwishoni mwa wiki katika mashambulizi ya Marekani na
Israel.
Israel yaanza mashambulizi mapya dhidi ya Tehran na Beirut
Chanzo cha picha, EPA
Jeshi la Ulinzi la Israeli (IDF) limethibitisha kwamba limeanzisha mashambulizi mapya katika mji mkuu wa Iran wa Tehran, pamoja na mji mkuu wa Lebanon wa Beirut.
"IDF kwa sasa inafanya mashambulizi yaliyolengwa kwa wakati mmoja dhidi ya maeneo ya kijeshi huko Tehran na Beirut," ilisema katika taarifa.
Msemaji wa IDF wa lugha ya Kiarabu Avichay Adraee alisema "wimbi la mashambulizi makubwa ya anga" linaendelea.
Mashambulizi hayo yametokea yapata saa moja baada ya IDF kutoa "onyo la dharura" kwa watu katika vitongoji vya kusini mwa Beirut na katika vijiji kadhaa, ikiwataka waondoke.
IDF ilikuwa imesema inalenga vituo vya amri na vituo vya kuhifadhia vitu vya Hezbollah.
Watanzania watahadharishwa safari za Mashariki ya Kati
Chanzo cha picha, Muskaan Kataria
Serikali ya Tanzania imesema inafuatilia kwa karibu hali ya usalama inayoendelea katika eneo la Mashariki ya Kati.
Serikali kupitia Wizara yake ya Mambo ya Nje, imeshauri raia wa Tanzania wanaoishi au wanaopanga kusafiri katika eneo hilo ikiwemo Bahrain,Israel,Kuwait,Qatar na Falme za Kiarabu (UAE) kuzingatia;
Kuepuka safari za kwenda au kutoka Mashariki ya Kati katika kipindi hiki.
Kubaki katika makazi wanayoishi inapowezekana.
Kufuata maelekezo yanayotolewa na mamlaka za maeneo husika na kuwa waangalifu wakati wote.
Kuepuka maeneo yenye shughuli za kiusalama au kijeshi katika maeneo wanayoishi.
Kutumia njia rasmi za mawasiliano na taarifa.
Kuhifadhi pasipoti na vitambulisho vya Tanzania katika sehemu salama na vitakapopatikana kwa urahisi iwapo kutakuwa na dharura.
Taarifa ya Wizara hiyo imesema pamoja na Misheni za Kidiplomasia, itaendelea kutoa taarifa na usaidizi wa Kibalozi kadiri hali itakavyoruhusu katika maeneo husika.
Rubio: Tuliishambulia Iran kwa sababu Israel ilikuwa karibu kushambulia na majeshi yetu yalikuwa hatarini
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Marco Rubio amesema katika akaunti mpya sababu ya kuanzisha mashambulizi ya kijeshi dhidi ya Iran.
Anasema kwamba Marekani ilipata taarifa kutoka kwa Israel kwamba ilikuwa inapanga mashambulizi ya kijeshi dhidi ya Iran, .
Washington imedai kwamba hatua hiyo ya Israel inaambatana na shambulio la mara moja la Iran dhidi ya majeshi ya Marekani, na kwa hiyo jeshi la Marekani lilianzisha operesheni ya kijeshi dhidi ya Iran kwa lengo la kuizuia.
Pia aliwaambia waandishi wa habari siku ya Jumatatu kwamba "dhamira" ya msingi ya mashambulizi ya Marekani dhidi ya Iran ni "kuharibu uwezo wao wa makombora ya balistiki ya [Wairani] wa kuyajenga pamoja na tishio ambalo jeshi lao la majini linaleta kwa meli za kimataifa."
Aliendelea kusema kuwa anatumai watu wa Iran wanaweza "kuiangusha" serikali hii na "kujenga mustakabali mpya wa nchi yao."
Bw. Rubio aliongeza kuwa "tungefurahi kama hili lingewezekana," lakini akasisitiza kuwa "lengo la misheni hii ni kuharibu uwezo wao wa makombora ya balistiki na uwezo wao wa majini."
Viongozi wa Israel nao wameeleza kuwa "kupinduliwa kwa utawala wa Jamhuri ya Kiislamu" ni moja ya malengo makuu ya mashambulizi yao ya pamoja na Marekani.
Bw. Rubio, ambaye pamoja na wadhifa wake wa Waziri wa Mambo ya Nje pia ni mshauri mkuu wa usalama wa taifa wa Donald Trump, alienda kwenye Bunge la Congress la Marekani Jumatatu ili kuwaeleza wawakilishi na maseneta wa Marekani sababu za kuanzisha vita na Iran.
Rwanda yaikosoa Marekani kuhusu vikwazo dhidi ya maafisa wake wa kijeshi
Chanzo cha picha, PAUL KAGAME/FLICKR
Rwanda imekosoa vikwazo vilivyowekwa na Marekani, ikiviita hatua hizo kuwa zisizo za haki na zenye upande mmoja huku kukiwa na mvutano unaoongezeka kuhusu mzozo mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Vikwazo hivyo vinalenga Jeshi la Ulinzi la Rwanda (RDF) na maafisa wakuu wa jeshi kwa madai ya kuunga mkono M23, kundi lenye silaha linalofanya kazi mashariki DRC.
Katika taarifa iliyotolewa Jumanne, Kigali ilisema hatua ya Marekani "inawakilisha vibaya ukweli na kupotosha ukweli" unaozunguka mzozo huo.
Kigali iliishutumu serikali ya DRC kwa kukiuka mara kwa mara makubaliano ya kusitisha mapigano kupitia mashambulizi ya ndege zisizo na rubani na mashambulizi ya ardhini.
"Mashambulizi ya ndege zisizo na rubani na mashambulizi ya ardhini yanayoendelea na yasiyo na mpangilio ni ukiukwaji wa wazi wa makubaliano ya kusitisha mapigano na DRC na yanaendelea kugharimu maisha ya watu wengi," taarifa hiyo ilisema.
Rwanda ilisisitiza kwamba lengo lake kuu ni usalama wa taifa, ikisema kwamba vitendo vya jeshi la Rwanda ni vya kujihami na vinalenga kukabiliana na makundi yenye silaha maadui wanaofanya kazi karibu na mipaka yake.
Rwanda ilidai zaidi kwamba Vikosi vya Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (FARDC) vinashirikiana na vikundi vyenye silaha vinavyoichukia Kigali, ikiwa ni pamoja na Kikosi cha Kidemokrasia cha Ukombozi wa Rwanda (FDLR).
Ingawa Washington inasisitiza kwamba vikwazo vinakusudiwa kukuza uwajibikaji na amani, Rwanda inasema kwamba utulivu wa muda mrefu unategemea kushughulikia kile inachokielezea kama chanzo kikuu,kuendelea kuwepo kwa makundi yenye silaha yanayoipinga Rwanda yanayofanya kazi ndani ya mashariki mwa Congo.
Majjibizano ya hivi karibuni ya kidiplomasia yanaangazia hali dhaifu ya juhudi za amani na vihatarishi tata vya kijiografia vinavyozunguka mzozo wa DRC.
Marekani yaweka vikwazo dhidi ya makamanda wa Rwanda wanaowaunga mkono waasi wa M23
Chanzo cha picha, AFP
Marekani imeweka vikwazo vikali kwa jeshi la Rwanda na makamanda wake wanne wakuu, ikiwashutumu kwa kuchochea migogoro katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Wizara ya Hazina inasema Jeshi la Ulinzi la Rwanda limekuwa likitoa mafunzo, kuandaa, na kupigana pamoja na kundi la waasi la M23, ambalo tayari limeidhinishwa na Washington na Umoja wa Mataifa kwa ukiukwaji wa haki za binadamu na kuhama kwa wingi mashariki mwa Congo.
Miongoni mwa wale wanaolengwa ni Vincent Nyakarundi, Mkuu wa Jeshi; Ruki Karusisi, kamanda wa Kitengo cha 5 cha ardhini, Mubarakh Muganga, Mkuu wa Jeshi la Ulinzi la Rwanda; na Stanislas Gashugi, mkuu wa Operesheni Maalum.
Mali zao nchini Marekani sasa zimezuiliwa, na raia wa Marekani wamezuiliwa kufanya biashara nao.
Hatua hiyo inakuja siku chache tu baada ya Marais Felix Tshisekedi wa DRC na Paul Kagame wa Rwanda kusaini Makubaliano ya Washington huko Washington, wakiahidi kukomesha uhasama.
Lakini muda mfupi baadaye, M23 iliteka Uvira, mji wa kimkakati kwenye mpaka wa Congo na Burundi, na kulazimisha maelfu kukimbia.
Marekani inasema usaidizi wa Rwanda umeruhusu M23 kuteka eneo, kushambulia vikosi vya Congo na Umoja wa Mataifa, na kupata ufikiaji wa maeneo yenye madini mengi.
Maafisa wanaonya kwamba kuendelea kuhusika kuna hatari ya kuiingiza kanda nzima ya Maziwa Makuu vitani.
Washington inasisitiza kwamba vikwazo hivyo havikusudiwa kuadhibu, bali kulazimisha kuzingatiwa kwa ahadi za amani. Rwanda bado haijasema chochote.
Watu 52 wauawa kwa mashambulizi ya Israel dhidi ya Hezbollah nchini Lebanon
Chanzo cha picha, EPA
Jeshi la Israel limesema limeshambulia maeneo ya Hezbollah nchini Lebanon, baada ya kundi la Shia linaloungwa mkono na Iran kusema kwamba lilirusha roketi na ndege zisizo na rubani katika mji wa Haifa wa Israel ili kulipiza kisasi cha mauaji ya Kiongozi Mkuu wa Iran Ayatollah Ali Khamenei.
Kitengo cha usimamizi wa majanga cha Lebanon kilisema watu 52 waliuawa na mashambulizi ya Israel nchini humo Jumatatu.
Hakukuwa na ripoti za majeruhi nchini Israel kutokana na shambulizi la Hezbollah, ambalo kundi hilo lilisema ni kulipiza kisasi kwa "damu safi" ya Khamenei na mashambulizi ya Israel nchini Lebanon tangu kusitisha mapigano kati yao miezi 15 iliyopita.
Waziri wa ulinzi wa Israel aliapa Hezbollah italipa "gharama kubwa".
Israel Katz alisema ameagiza jeshi la Israel “kuchukua hatua kali” dhidi ya wanamgambo na chama cha kisiasa cha Hezbollah, na kwamba kiongozi wake, Naim Qassem, sasa ni “lengo lililowekewa alama ya kuondolewa.”
Waziri Mkuu wa Lebanon, Nawaf Salam, alilaani hatua za Hezbollah kuwa “zisizo za kuwajibika” na kusema serikali yake inapiga marufuku mara moja shughuli za kijeshi za kundi hilo.
Ilikuwa imetarajiwa kwa kiasi kikubwa kwamba Hezbollah, ambayo ina uhusiano wa karibu wa kifedha na kiitikadi na Iran, ingejiunga na mzozo kati ya Iran, Israel, na Marekani.
Mzozo huo umeenea kwa kasi katika Mashariki ya Kati tangu shambulio la pamoja la Marekani na Israel dhidi ya uongozi na majeshi ya Iran siku ya Jumamosi, huku Iran ikijibu kwa kurusha makombora na ndege zisizo na rubani kuelekea Israel na mataifa ya Kiarabu ya Ghuba yanayohifadhi vituo vya kijeshi vya Marekani.
Watu wasiopungua 169 wauawa katika shambulio la 'kushtukiza' Sudani Kusini
Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
Mamlaka nchini Sudan Kusini zimesema watu wasiopungua 169, wakiwemo maafisa wakuu, waliuawa Jumapili wakati kundi la watu wasiojulikana walipoanzisha shambulio katika eneo moja kaskazini mwa nchi.
Akielezea shambulio hilo linalodaiwa kufanywa na vijana kadhaa wenye silaha, Waziri wa Habari wa Eneo la Utawala la Ruweng, James Monyluak Mijok, alidai kwamba walitoka katika jimbo jirani la Unity na walikuwa na uhusiano na Jeshi la Ukombozi wa Watu wa Sudan katika Upinzani (SPLA-IO).
SPLA-IO imekana kuhusika kokote katika shambulio hilo, ikishutumu mamlaka ya jimbo la Unity kwa kuingilia vurugu hizo kisiasa.
Umoja wa Mataifa umeonya mara kwa mara kwamba nchi iko katika hatari ya kurudi kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe.
“Waliokufa ni pamoja na watoto 90, wanawake na wazee, pamoja na maafisa 79 wa vikosi vya kikanda, wakiwemo polisi,” Mijok alisema.
Mijok aliiambia BBC kwamba washambuliaji waliingia kaunti ya Abiemnom katika eneo la Ruweng kabla ya alfajiri Jumapili, takribani saa 4:30 asubuhi kwa saa za huko (02:30 GMT), wakati watu bado walikuwa wamelala na “waliwashitukiza”.
Alisema kuwa vikosi vya serikali vilivyokuwa eneo la tukio “vilizidiwa idadi… Washambuliaji walichoma moto nyumba na masoko wakati wa mapigano yaliyodumu kati ya saa tatu hadi nne.” Maafisa kadhaa waandamizi wa eneo hilo waliuawa, akiwemo kamishna wa kaunti na mkurugenzi mtendaji.
Mijok alisema tangu wakati huo vikosi vya serikali vimewafurkuza washambuliaji na kwamba sasa mamlaka zina udhibiti kamili wa eneo hilo.
Netanyahu adai kuwa ingekuwa vigumu kwa mpango wa nyuklia wa Iran kudhibitiwa
Chanzo cha picha, Getty Images
Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, ametetea mashambulizi ya kijeshi ya Israel dhidi ya Iran, akidai kwamba ongezeko la hivi karibuni la mpango wa nyuklia wa Tehran “lisingekuwa rahisi kudhibiti ndani ya miezi michache” kabla ya hatua ya Israel.
Licha ya mashambulizi ya pamoja ya anga ya Israel na Marekani yaliyolenga vituo vitatu vya nyuklia wakati wa vita vya siku 12 mwezi Juni, Netanyahu anasema wanajeshi na mafundi wa Iran walianza kujenga maeneo mapya, yakiwemo “ya chini ya ardhi,” ambako wangeweza kuendeleza makombora ya balistiki na mabomu ya atomiki.
“Kama hakuna hatua ingechukuliwa sasa, basi hakuna hatua ambayo ingeweza kuchukuliwa baadaye,” Netanyahu aliiambia Fox News.
Israel kwa muda mrefu imepinga urutubishaji wa nyuklia wa Iran, ikionya kuwa unaweza kutumika kutengeneza silaha za nyuklia badala ya kutumika kwa madhumuni ya amani kama inavyodai serikali ya Iran.
Ubalozi wa Marekani Saudi Arabia washambuliwa na ndege zisizo na rubani
Chanzo cha picha, Reuters
Wizara ya Ulinzi ya Saudi Arabia imethibitisha kwamba ubalozi wa Marekani mjini Riyadh ulishambuliwa na ndege mbili zisizo na rubani, kulingana na makadirio ya awali.
Katika taarifa iliyochapishwa kwenye mtandao wa X, wizara hiyo ilisema hii ilisababisha "moto mdogo na uharibifu mdogo wa vifaa kwenye jengo hilo".
Ubalozi wa Marekani umewaagiza wafanyakazi wake walioko Saudi Arabia kubaki ndani katika miji ya Jeddah, Riyadh, na Dhahran kutokana na uwezekano wa tishio la kiusalama.
Ujumbe huo utapunguza au utaepuka safari zisizo za lazima kwenda kwenye vituo vya kijeshi katika eneo hilo, kama tahadhari kwa sababu za usalama.
Donald Trump alikiambia kituo cha runinga cha NewsNation kwamba Marekani italipiza kisasi “hivi karibuni” kufuatia shambulio dhidi ya ubalozi wa Marekani mjini Riyadh na vifo vya wanajeshi wa Marekani.
Wanajeshi sita wa Marekani wameuawa hadi sasa huku 18 wakiwa wamejeruhiwa, Marekani ilisema Jumatatu usiku.