Klabu ya Wasichana wapweke: 'Niliona watu kwenye skrini pekee'

Na Sarah Hawley

BBC News, Nottingham

Nusu ya watu wa Uingereza wanakiri kujihisi kutengwa wakati fulani, huku 7% ya wanawake wakiripoti hisia za upweke wa kudumu. Lakini jumuiya mpya ya "wasichana wapweke" imedhamiria kuthibitisha kuwa hawako peke yao.

Ni Ijumaa usiku. Wakati ambapo watu wengi huchangamkia wikendi ijayo. Lakini si Charelle Griffith mwenye umri wa miaka 35.

"Nachukia wazo hili la kufanya kazi kwa bidii sana, ikifika mwisho wa wiki, Ijumaa usiku na nitakuwa ndani ya nyumba peke yangu. Sio hisia nzuri."

Charelle ambaye ni mzungumzaji na mwenye hulka ya uchangamfu - anakiri ,mwenyewe kuwa si mtu anayependa kuchangamana na watu wengi , akiendesha biashara yake ya kibinafsi katika eneo la Nottingham mjini London.

Anasema pia huwa anajipata katika nyakati za upweke uliokithiri, akisema kuwa huona aibu ya kuchangamana na watu.

"Watu hawatarajii mimi kuwa mimi ninaweza kuwa mpweke," alisema. "Wananiambia 'lakini daima una furaha na tabasamu', lakini kuna njia tofauti unaweza kujihisi mpweke.

"Nina marafiki wazuri ambao wanaishi kote nchini lakini kwa upande wa mtu huko Nottingham ambaye ningeweza kumtembelea na kuwa na wakati mzuri naye, ndiyealiyekosekana maishani mwangu."

Klabu ya kwanza ya Wasichana ya Upweke ilianzishwa London

Charelle aligundua kuwa alikuwa akikabiliana na upweke mwaka wa 2021. Wakati wa janga la Covid alikuwa amefukuzwa kazi katika West End London.

Alirudi katika mji wake wa nyumbani ili kuanzisha biashara yake mwenyewe, lakini sheria ya Covid ya kujitenga ilikuwa ngumu.

"Nilitoka katika hali ya kuwa kazini ambapo nilikuwa karibu na watu kila siku," alisema. "Nilikuwa nikienda kwenye ukumbi wa michezo na mitandao nyakati za jioni, mara nyingi nikitumia siku peke yangu na kuona watu kwenye skrini pekee. Sidhani kama ni rahisi kupata marafiki wapya ukiwa mtu mzima."

Uzoefu wa Charelle sio wa kipekee . Mhitimu Holly Cooke pia alipambana na upweke baada ya kufuata "ndoto yake kubwa" za kuhamia London - na aliamua kutafuta njia ya kujisaidia yeye na wengine.

"Nilifika hapa na sikujua mtu hata mmoja, sikuwa na mtu yeyote wa kwenda naye kula chakula cha mchana au kwenda naye kwenye ukumbi wa michezo, na hali hii iliniingiza katika upweke haraka," alisema.

Klabu ya wenye upweke,The Lonely Girls Club, ilitokana na "hitaji la kibinafsi la Holly la kuungana na marafiki na kutafuta watu wa kubarizi nao".

Aliianzisha kwenye mtandao wa Facebook miaka mitano iliyopita, na sasa wanachama hupanga matukio mbali mbali mjini London.

Kwa sababu ya umaarufu wake, tawi jipya lilianzishwa huko Manchester. Tangu wakati huo, klabu hiyo imekua "kwa kiasi kikubwa" na sasa ina wanachama 70,000 - wenye umri wa kuanzia 18 hadi 60.

Vikundi zaidi sasa vinaundwa kote nchini.

Holly anasema: "Upweke huja kwa maumbo na ukubwa mbalimbali na unaweza kuathiri watu katika sehemu mbalimbali za maisha yao, katika umri mbalimbali... na kwa sababu mbalimbali.

"Unaathiri maeneo yote ya maisha yako, afya yako ya akili, afya yako ya mwili, motisha yako ya kutoka na kufanya mambo, na unaweza kusababisha athari kujumuisha kwa ujumla."

'Nyanja zote za maisha'

"Nadhani hamu hii ya urafiki, hitaji hili la kujumuika na watu wengine ni jambo ambalo watu wanafurahia zaidi kulizungumzi na kusema 'ndio niko mpweke lakini sitaki kuishi mpweke', na tuko hapa kusaidia hilo," Holly aliongeza.

Charelle, ambaye alijiunga na tukio la kwanza la Nottingham la Lonely Girls Club mnamo Januari, anaamini kuwa inasaidia "kurekebisha" upweke.

"Badala ya kujisikia kama wewe ndiye mtu pekee mpweke katika jiji, na kujihisi vibaya zaidi, badala yake kwa kweli unagundua kuna watu wengi ambao pia wana upweke," anasema na kuongeza kuwa 'baada ya kujiunga na klabu hii inakufanya uwe mwenye mawazo chanya kusema kweli''

"Kulikuwa na aina mbalimbali za watu huko na kutoka kila sekta ya maisha," aliongeza.

"Ninapenda kucheza dansi na kukutana na watu wengine wanaopenda kucheza. Ninahisi kama nitapata watu ninaoungana nao na ninaoweza kufanya nao mambo ya kujifurahisha. Nilikuwa na wakati mzuri."

Imetafsiriwa na Dinah Gahamanyi