Pakistan yaanzisha mashambulizi dhidi ya Afghanistan, Taliban yasema makumi ya watu wameuawa

Chanzo cha picha, EPA/Shutterstock
Pakistan imefanya mashambulizi mengi ya anga usiku kucha nchini Afghanistan, ambayo Taliban imesema yameua na kujeruhi watu kadhaa, wakiwemo wanawake na watoto.
Islamabad ilisema mashambulizi hayo yalilenga kambi saba zinazodaiwa kuwa za wanamgambo na maficho karibu na mpaka wa Pakistan na Afghanistan na kwamba yalianzishwa baada ya mabomu ya kujitoa mhanga hivi karibuni nchini Pakistan.
Afghanistan ililaani mashambulizi hayo, ikisema yalilenga nyumba nyingi za raia na shule ya kidini.
Mashambulizi hayo mapya yanakuja baada ya nchi hizo mbili kukubaliana kusitisha mapigano kwa muda mwezi Oktoba kufuatia mapigano makali ya mpakani.
Wizara ya ulinzi ya Taliban ilisema mashambulizi hayo yalilenga maeneo ya raia wa majimbo ya Nangarhar na Paktika. Maafisa wa Nangarhar waliiambia BBC kwamba nyumba ya mwanaume anayeitwa Shahabuddin ilipigwa na moja ya mashambulizi hayo, na kuua takriban wanafamilia 20, wakiwemo wanawake na watoto.
Mashambulizi ya hivi karibuni nchini Pakistan yalijumuisha moja kwenye msikiti wa Shia katika mji mkuu Islamabad mapema mwezi huu, pamoja na mengine yaliyotokea tangu mwezi mtukufu wa Ramadhani uanze wiki hii katika jimbo la kaskazini-magharibi la Khyber Pakhtunkhwa.
Pakistan iliwashutumu Taliban wa Afghanistan kwa kushindwa kuchukua hatua dhidi ya wanamgambo hao, ikiongeza kuwa ilikuwa na "ushahidi kamili" kwamba mashambulizi hayo yalifanywa na wanamgambo kwa maagizo ya uongozi wao nchini Afghanistan.






